Breaking

Thursday 23 June 2022

TRC YATAJA SABABU AJALI YA TRENI TABORA, YASEMA NI HUJUMA


Chanzo cha ajali ya treni ya abiria iliyotokea jana Juni 22, 2022 Mkoani Tabora na kusababisha vifo vya watu kadhaa na kujeruhi wengine kimetajwa kuwa ni hujuma.

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kuna kipande cha reli kiliondolewa na kisha kurudishwa kwa kuegeshwa ili kisionekane kama kimeegeshwa.

Kadogosa amebainisha kuwa mwendo wa treni hiyo ulikuwa mdogo na kama ungekuwa wa kasi kubwa basi madhara yangekuwa makubwa zaidi kwa vifo na majeruhi.

"Eneo lililopata ajali treni hiyo lipo jirani na makazi ya watu na mara zote treni za abiria na mizigo huwa zinapita kwa mwendo wa pole," amesema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Honoratha Rutatinisibwa amesema bado wanaendelea kuhesabu waliofariki na majeruhi wa ajali hiyo.

Honoratha hakutaka kujibu kama waliofariki ni wanne au watatu akibainisha kuwa wanaendelea kuhesabu ingawa mmoja wa watumishi wa hospitali ya Kitete aliyeomba kuhifadhiwa ya jina lake amesema waliofariki ni zaidi ya wanane.



Source: Mwananchi
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages