Breaking

Thursday 24 November 2022

AJALI YA MOTO YATEKETEZA BWENI NA KUUA WATOTO WATATU WENYE ULEMAVU BUHANGIJA

Muonekano wa Bweni lililoteketea kwa moto na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija mkoa wa Shinyanga.

**********

Moto ambao haujajulikana chanzo chake umeunguza bweni la Kituo cha Kulelea Watoto wenye ulemavu cha Buhangija Mjini Shinyanga na kusababisha vifo vya watoto watatu wa kike wenye ulemavu wa macho.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema moto huo umetokea Novemba 23,2022 majira ya saa nane usiku katika bweni B lililokuwa na watoto 32 katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu (watoto wenye ualbino, viziwi na wasioona).

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linafanya uchunguzi wa tukio la moto ambao haujafahamika chanzo chake na kuteketeza bweni katika kituo cha kulelea watoto walemavu Buhangija kilichopo mkoa wa Shinyanga na kusababisha vifo vya watoto watatu wa kike”,amesema Kamanda Magomi.

Amewataja watoto waliofariki dunia kuwa ni Miliam Limbu (12), mwanafunzi wa darasa la pili, Caren Mayenga (10), Catherine Paulo (10) wote ni walemavu wa macho (wasioona), wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi Buhangija.

Amesema kufuatia tukio hilo mali mbalimbali za wanafunzi na za shule zimeharibika ambazo bado thamani yake haijafahamika na hakuna majeruhi yeyote.


“Baada ya taarifa za tukio hili kupatikana Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio, Pia jeshi la zimamoto na uokoaji nalo lilifika katika eneo la tukio na kufanikiwa kuzima moto ule pamoja na TANESCO kufanikisha uzimaji wa umeme haraka katika eneo lile ili kuzuia madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea kutokana na moto ule”,ameeleza Kamanda Magomi.

Amefafanua kuwa kituo cha kulelea watoto Buhangija kilikuwa na watoto 163 waliolala bwenini kituoni hapo siku ya tukio ambapo watoto wenye ualbino ni 77 kati yao wa kike 38, wa kiume 39, wasioona 20 wa kiume 9, kike 11 ambapo watatu wamefariki dunia na Viziwi 66 kati yao wa kiume ni 31 na wa kike 35.

Soma zaidi >>HAPA<<
Via: Malunde 1 Blog
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages