Breaking

Monday 28 March 2022

WAKURUGENZI WATAKIWA KUJENGA MATUNDU YA VYOO VYA SHULE KUPITIA FEDHA ZA NDANI




WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutenga fedha na kuweka kipaumbele cha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari kupitia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.


Waziri Bashungwa Ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Machi 28, 2022 wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Bungene iliyopo Wilaya Karagwe mkoani Kagera na kukuta upungufu wa matundu ya vyoo ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo.


Amesema baada ya Rais Samia kuelekeza fedha za mkopo wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika ujenzi wa madarasa 12,000 ambayo yamepunguza msongamano na wanafunzi kutembea mwendo mrefu, sasa changamoto imebaki kwenye upungufu wa matundu ya vyoo shuleni.


Waziri Bashungwa amesema, katika jitihada za kupunguza uhaba wa madarasa katika Shule ya Sekondari Bugene, Serikali italeta fedha za kujenga vyumba vya madarasa manne na kutenga bajeti ya kufanya ukarabati wa madarasa na mindombinu iliyochakaa.


Aidha Waziri Bashungwa amesema, Serikali itatoa fedha kujenga bweni moja ili kupunguza upungufu wa mabweni mawili katika shule hiyo ya Sekondari ya Bugene.


Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bugene, Asia Rupia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu, miundombinu mbalimbali na kugharamia elimu bila malipo ambapo shule inapokea shilingi milioni 20.1 kila mwezi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages