Breaking

Sunday 20 March 2022

WANACHI WATAKIWA KUFUATA NJIA SAHIHI KULINDA AFYA YA KINYWA NA MENO

 


Wananchi wameaswa kulinda afya zao za Kinywa na meno kwa kufuata njia sahii za kujikinga.

 

Hayo yamesemwa leo Jumapili Machi 20, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoani Ruvuma.


Prof. Makubi amesema swala la kujikinga na Magonjwa ya Kinywa na Meno ni muhimu zaidi kuliko kusubiri kuingia kwenye hatua ya matibabu.


"Usafishaji wa kinywa kwa usahihi, matumizi ya miswaki yenye sifa stahiki, na udhibiti wa ulaji wa vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kufanya uchunguzi wa Kinywa na Meno walau mara moja kwa mwaka ni miongoni mwa mambo ya msingi na ya lazima ili kuwa na Kinywa chenye Afya njema" Amesema Prof Makubi . 



Amesema matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku pamoja na unywaji wa pombe uliopitiliza huchangia kupata madhara ya magonjwa ya fizi, saratani kwenye ulimi, mdomoni na koo.


Ametumia maadhimisho hayo kuwahimiza wananchi Kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili kuweza kupata huduma kwa gharama nafuu na haraka.


"Wito wangu kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na taifa nzima tuendelee kujitokeza kwa hiari kujiunga na mfuko wetu wa bima ambao utasaidia kuboresha huduma zetu na kupata huduma bora " Amesema Prof. Makubi



Aidha, Prof. Makubi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha huduma ya Kinywa na Meno zinaimarika, kwa kuendelea kununua vifaa tiba vya kisasa na kuboresha miundombinu ya matibabu hayo katika hospitali na vituo vya afya.


"Takwimu zinaonyesha jumla ya Wagonjwa 685,224 walihudhuria kwa ajili ya  matibabu ya Kinywa na Meno katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya kwa mwaka 2021, Wagonjwa 506,950 (74%) walikuwa na tatizo la kutoboka kwa meno ilihali watu 69,318 walikuwa na Magonjwa ya Fizi."Prof.Makubi




Kwa upande mwingine Prof. Makubi amemshukuru Rais wa awamu ya sita Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za afya zina imarika kwa kuendelea kununua vifaa vya kisasa, kujenga miundombinu na kuboresha matibabu kwa ujumla.


"Kwenye fedha za Uviko - 19 uwekezaji mkubwa umefanyika katika vituo vyetu vya afya kwa kujenga vyumba vya kutibu wagonjwa mahututi na dharura pamoja na vifaa vya kisasa" Amesema Prof Makubi.


MWISHO.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages