Breaking

Monday 16 May 2022

HATMA YA WABUNGE 19 CHADEMA KUAMULIWA NA MAHAKAMA





Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DKt.Tulia Ackson amesema kwa sasa hawezi kutamka kuwa viti 19 vya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliofukuzwa uanachama vipo wazi, kwani suala hilo lipo mahakamani.

Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 16, 2022 bunge jijini Dodoma kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki ni mahakama.

Amesema kwa kuwa tayari alipokea barua kutoka kwa wabunge hao 19 wakimtaarifu kuwa tayari wamefungua shauri mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama.

"Bunge haliwezi kuingilia mchakato wa mahakama na badala yake linalazimika kusubiri hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi wake" Amesema Spika Tulia

Tarehe 11 mwezi huu Baraza Kuu la CHADEMA lilitupilia mbali rufaa ya wabunge hao ambao walikuwa wakipinga kufukuzwa uanachama na Kamati Kuu ya chama hicho, na hivyo kumlazimu Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika kuwasilisha barua kwa Spika kumtaarifu kuhusu jambo hilo ili aendelee na taratibu nyingine.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages