Breaking

Friday 27 May 2022

WAZIRI MCHENGERWA ATEMA CHECHE KWA VIONGOZI WA MICHEZO, ATAKA WABADILIKE


Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa amewataka  viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini kutotumia taasisi wanazoziongoza kujinufaisha kwa  vipato tu na badala yake wawe wabunifu na wazalendo ili kuleta  mapinduzi kwenye  michezo.


 Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Mei 27, 2022 wakati akifunga  kikao kazi cha viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini  kilichoratibiwa  na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kufuatia  maelekezo yake aliyoyatoa wakati akiisimika Bodi  ya BMT hivi karibuni ya kutaka kuwa na utawala bora kwenye vyama na mashirikisho ya michezo ili kuendeleza michezo.


 Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa yapo  mataifa  mbalimbali duniani ambayo  hayana miundombinu ya michezo na  yana idadi ndogo ya watu ukilinganisha  na Tanzania  lakini yamekuwa yakifanya  vizuri kwenye  michezo hivyo amewataka kubadili fikra  potofu ili wanaowaongoza waige  mifano kutoka  kwao hatimaye kuleta mapinduzi makubwa kwenye michezo. 


 “Hatutaweza kupiga hatua kwenye michezo kama   sisi viongozi hatutaweza kubadilika na kuendelea kuwa na fikra potofu ya kudhani vyama na mashirikisho ni mahali pa kujipatia vipato tu. Nawaomba tubadilike mimi katika kipindi changu sitaweza kuruhusu kutokea hayo. Mpango wa matumauni ya kesho lazima tuanze kujenga leo”. ameongeza Mhe. Mchengerwa.


Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu kubwa kuendeleza sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo maana iliunda upya Wizara hii ili iweze kujitegemea, kuongeza bajeti, kutoa punguzo kwenye nyasi bandia ili kuimarisha viwanja vya soka pamoja na kuanzisha mfuko wa maendeleo ya michezo.


Ameongeza kuwa mfuko huo umepewa chanzo madhubuti ambacho  ni fedha za asilimia tano ya mapato yatokanayo na michezo ya kubashiri matokeo ya michezo.


Kikao hicho pamoja na mambo mengine kimejadili kwa kina vigezo   vya muongozo wa kusaidia timu za taifa  kwa kutumia fedha za mfuko wa maendeleo ya michezo na kuja na mawazo ambayo yatafanyiwa  kazi na serikali ili kuwa na uwazi katika usaidiaji wa  timu hizo katika michezo mbalimbali.  


Aidha, amewasihi viongozi hao kufuata  miongozo na taratibu za nchi  sambamba na kuziheshimu  mamlaka  na taasisi zinazosimamia michezo nchini,  kuimarisha  utawala bora na weledi  katika kazi.


Mambo mengine ni pamoja na kuimarisha eneo la utaalamu na taswira za    taasisi zao kwa kuwa na mikakati yenye dira.


Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kujenga miundombinu mipya na ya kisasa ya michezo ambapo kwa upande wake Naibu Waziri, Mhe, Pauline Gekul amewataka wadau washirikiane na kupendana ili kuongoza kwa mafanikio.


Naye Katibu Mkuu. Dkt, Hassan Abbasi amewataka viongozi hao kuwa wabunifu wa kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato badala ya kutegemea Serikali pekee.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages