Breaking

Saturday 11 June 2022

VIDEO: ASKARI AUAWA LOLIONDO, RC MONGELLA ATHIBITISHA


Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella amesema askari mmoja amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kupigwa mshale na kundi la watu wenye silaha wakati wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro.

Pia, amesisitiza kuwa hali ya Loliondo ni shwari na uwekezaji wa mipaka katika eneo la kilometa 1,500 kwa ajili ya eneo nyeti la mazalia, chanzo cha maji na mapito ya wanyama kwenye eneo hilo.

Mongolla ameeleza hayo leo Jumamosi ya Juni 11, 2022 wakati akizungumzia kuhusu kinachoendelea katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro.

Mongella amesema kuwa kwa bahati mbaya jana alasiri askari mmoja aliuawa kwa kupigwa mshale na kundi la watu ambao lilitokea na kutaka kuathiri zoezi hilo na hata kuathiri utekelezaji wa zoezi hilo.

“Kwa bahati mbaya tu, alasiri ya jana (Ijumaa ya Juni 10, 2022) askari wetu mmoja aliuawa kwa kupigwa mshale na kundi la watu ambalo lilitokea na kutaka kuathiri na hata kuumiza wanaondelea na zoezi.

“Ni bahati mbaya sana, lakini askari huyu mzalendo tunatambua mchango wake na pamoja na kauli nzuri ya Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) bungeni jana asubuhi, lakini alasiri tulipata tukio hilo,” amesema Mongella.


Amesema kuwa kwa sasa zoezi hilo linaendelea vizuri na kwamba, baada ya kuweka alama kwenye maeneo hayo ni kuwa, mazoezi hayo yatakuwa shiriki kwa wananchi wote.

Amesema mpaka sasa kwenye maeneo na hospitali na vituo vya afya hakuna majeruhi, ingawa kwenye mitandao kuna picha zinatolewa na baadhi ni za miaka mingi iliyopita.

Jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilieleza Bunge kuwa kumekuwa na upotoshaji kuhusu kinachoendelea katika Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro na kuwataka wale wanaofanya hivyo watafutwe.

Majaliwa alisema kinachofanyika ni uwekezaji wa alama kwenye maeneo ya mipaka ya wanyama na vyanzo vya maji na kwamba zoezi linakwenda vizuri hivyo, madai ya kuwepo vurugu kati ya wananchi na vikosi vya dola ni upotoshaji.

Majaliwa aliagiza kusakwa kwa wote wanaosambaza taarifa hizo za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii ili hatua kali za kisheria zilichukuliwe dhidi yao.

Hata hivyo, tangu juzi na jana kumekuwa na picha na video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wananchi wa jamii ya kimasai wakijiandaa kuwakabili askari wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mapanga na mishale.

Mbali na hizo pia, kumekuwepo picha zikionyesha baadhi ya watu wakiwa wamejeruhiwa ambazo zinadaiwa kuwa ni za Loliondo.

Hata hivyo, Mongela amewataka wote waliojeruhiwa kujitokeza na kupatiwa matibabu huku akieleza kuwa, hakuna mtu aliyejeruhiwa kwenye vituo vya afya na hospitali wilayani humo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages