Breaking

Wednesday 15 June 2022

BALOZI POLEPOLE AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA MALAWI



Lilongwe, Malawi


Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Nancy Tembo kuangalia namna gani wanaweza kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kiuchumi, kibiashara na ujirani mwema.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatano Juni 15, 2022 pia yalijikita katika kuangalia namna watakavyofanya vikao vya pamoja vitakavyokuza na kuendeleza mahusiano baadaye mwaka huu.


Hilo pia litaenda sambamba na kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya maendeleo ambayo iyokwishakubaliwa baina ya Tanzania na Malawi.

“Nikuhakikishie kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza na kukuza mahusiano imara na madhubuti yaliyopo na ambayo yamekuwa yakiwanufaisha kiuchumi na kimaendeleo wananchi wa pande zote mbili, Tanzania na Malawi,” amesema Polepole.

Pia Polepole amepokea ujumbe wa walimu 21 wa shule za awali, msingi na sekondari kutoka Zanzibar ambao waliopo katika ziara ya mafunzo kwa vitendo nchini Malawi.

“Ubalozi umejipanga pamoja na mambo mengine katika uhusiano wa Tanzania na Malawi pia tunataka kukisogeza Kiswahili nchini Malawi ili kitumike kwa watoto, vijana na wananchi wa Malawi kwa ujumla,” amesema Polepole.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages