Breaking

Wednesday 1 June 2022

UMATI YALAANI VITENDO VYA KIKATILI KWA WATOTO, YAIOMBA SERIKALI KUDHIBITI



Dar es Salaam 

Kufuatia kuongezeka kwa matukio mengi yanayoripotiwa na vyombo vya habari pamoja na vyombo vya dola hapa nchini kuhusiana na hali ya ukatili unaoendelea kutokea miongoni mwa jamii hasa ubakaji na ulawiti kwa watoto, Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) kimepinga na kulaani vikali vitendo wanavyofanyiwa watoto ambavyo vinaripotiwa kuongezeka hapa nchini.


Akizungumza na Waandishi wa habari leo Mei Mosi, 2022 Mwenyekiti wa Taifa na Mwenyekiti wa bodi ya UMATI Sheikh Swed Twaibu Swed amesema kuwa vitendo hivo vimekua vikileta taharuki , wasiwasi, magonjwa na hata vifo kwa baadhi ya wahanga wa vitendo hivo.


Amesema vitendo vya ukatili sio tu vinaharibu na kukatisha ndoto za vijana wengi ambao hukata tamaa baada ya kufanyiwa vitendo hivo pia vinadhalilisha jamii ya Tanzania ambayo imekua ni mfano wa malezi bora ya watoto kwa muda mrefu.


" matokeo ya hali ya vitendo vya ukatili imewafanya vijana wengi kutofahamu wapi waende kuripoti mara tu wanapokutana na ukatili wa aina yoyote kwa kuwa mara nyingine ukatili unatokea ndani ya familia " Amesema Sheikh Swed


Kufuatia hali hiyo chama hicho kupitia Mwenyekiti wake kimetoa wito kwa Serikali kuhakikisha inasimamia maeneo yote muhimu hasa katika mambo ya kijamii kuanzia ngazi ya Kijiji hadi kata ambapo vitendo hivyo vinafanyika na Maafisa wa Ustawi wa Jamii na Maafisa Afya wako kila Kata.


Pia wameliomba jeshi la Polisi kupitia madawati maalumu kuwapokea kwa weledi waathirika ili wasipate wasiwasi wa kusambaa kwa habari hizo.



Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania ( UMATI) , Suzana Mkanzabi amewataka Wazazi kujenga tabia ya kujenga urafiki na vijana wao na kuzungumza nao kila wakati badala ya kuwa na dhana ya kuwa watoto wao hawajui chochote.


Ameongeza kuwa ili kuondokana na changamoto hizo UMATI kwa kushirikiana na wadau wengine inaratibu afua zinazowawezesha vijana balehe, Wanawake walio kwenye ndoa na watu wanaoishi na ulemavu kutambua haki zao na kutovumilia viashiria vya ukatili wa aina yoyote na kuripoti kwenye mamlaka husika kama dawati la Jinsia au uongozi wa Kijiji.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages