Breaking

Thursday 30 June 2022

WAZALISHAJI WA WINE WILAYANI KARAGWE MKOANI KAGERA WAJIVUNIA UTOAJI AJIRA KWA VIJANA , RAIA WA BURUNDI WAFUNGUKA

Na Lydia Lugakila, lango la habari


Kauli hiyo imetolewa na Yesse Kagenzi afisa habari na uhusiano kutoka kampuni ya HLUCY &MARTINE BEVERAGE CO.LTD ambao ni wazalishaji wa wine kwa kutumia viungo , mimea na matunda mbali mbali wakati akiongea na  lango la habari katika maonyesho ya kwanza kibiashara ya jumuiya ya Afrika mashariki yanayoendelea katika viwanja vya CCM manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera


Kagenzi amesema kuwa wamewiwa kujumuika katika maonyesho hayo ili kutangaza vyema bidhaa zao kitaifa na kimataifa ikiwemo na kutoa elimu kwa vijana wengi, lengo likiwa ni kuwainua vijana kujitambua na kuchangamkia fursa zilizopo katika viwanda ikiwa tayari wamejipambanua katika kutoa ajira kwa vijana wengi nchini.


Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho  mwaka 2018 wameamua kushirikiana na serikali kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kuwaajiri vijana kwa asilimia 30 huku akiwahimiza vijana kutumia nguvu zao, uwezo wa mawazo,  ubunifu ikiwemo kutokata tamaa badala yake wapambane katika kutafuta maisha.


Ametumia maonyesho hayo ya kibiashara kuwahimiza wakulima wa tangawizi, mchai chai mdalasini na mimea mingine inayotumika kutengeneza wine hiyo wilayani Karagwe kulima kwa wingi mazao hayo ili kupata fursa ya kuuza kiwandani hapo na kujipatia kipato .


Akielezea kiwanda hicho cha kuzalisha wine amesema kinapatikana wilayani Karagwe Mkoani Kagera kinazalisha wine kwa kutumia viungo, mimea na matunda mbali mbali kama Rosela, Mdalasini, Mlonge, Mchai chai Kaswagara, zabibu kavu na karafuu huku akiishukuru serikali pamoja na waandaaji wa maonyesho hayo kwani tayari wameongeza elimu ya biashara.


Aidha katika hatua nyingine  mfanya biashara  kutoka nchini Burundi aitwaye Minani Floribert ambaye pia ni mwana kikundi cha sanaa na muuzaji wa bidhaa zitokanazo na kazi za mikono  ametaja kuvutiwa na maonyesho hayo yaliyoendana na elimu ya biashara huku akieleza kunogewa hadi kusahau nyumbani Burundi.


"Kilichonifurahisha kwa hapa Tanzania ni muitikio  mkubwa kwenye masuala ya biashara wana Kagera wanapenda kazi za mikono, viongozi wanapenda kuinua wana sanaa, huduma ni nzuri natamani kila mwaka maonyesho hayo yawepo hakika tumepasahau Burundi" alisema Minani.


 ametumia fursa hiyo kuwaomba vijana wa kitanzania kujiajiri katika kazi mbali mbali za mikono ili wajitegemee wenyewe.


Ameiomba serikali hapa nchini kuwashika mkono vijana wa Kitanzania kwa kuwawezesha vifaa vya kufundishia kazi za mikono huku akiahidi kutoa mafunzo hayo mwenyewe na kusisitiza vijana kujifunza sanaa ya Burundi manufaa yao na taifa kwa ujumla.


Maonyesho hayo ya kibiashara ya jumuiya ya Afrika mashariki yalianza  juni 15 mwaka huu na kufunguliwa rasmi juni 25 yatafungwa julai 10, 2022.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages