Breaking

Friday 22 July 2022

HUYU NDIYE KING KIBADEN SHUJAA ASIYESAHAULIKA SIMBA SC


Na Mwandishi Wetu

MMOJA wa Watanzania ambao wamefanya mambo ambayo hayawezi kusahaulika katika nchi hii ni Abdallah Athuman Seif maarufu Abdallah King Kibadeni Mputa, ama Ndururu.


Katika mahojiano aliyofanya na mwandishi wetu hasa yakilenga miaka 45 ya kipigo kisichosahaulika cha mabao 6- 0 ilichokitoa Simba SC kwa watani zao Yanga Afrika katika mchezo wa ligi tarehe 19 ya mwezi Julai mwaka 1977, mzee Kibaden aliongelea masuala mbalimbali ya soka na pia akigusia kuhusu historia yake binafsi.


Anaelezea kuwa jina lake halisi ni Abdallah Athuman Seif na ni mzaramo kwa mama yake mzazi na kwa baba ni mngindo.


Anadai jina hili la Kibaden lilikuja tu na wala si la kuzaliwa,jina lake halisi ni Abdallah Athuman Seif na hivyo kufafanua baba yake mzazi ni marehemu Athuman Seif.


Jina hili la Kibaden limetokea wapi?

Alipoulizwa sababu haswa ya yeye kuitwa Kibaden na badala ya jina lake halisi la Abdallah Athuman Seif, mzee Kibaden anadai kuwa jina hili alipewa wakati akiwa anasoma madrasa wakati wa udogo wake vijana wenzake wakati huo walikuwa wakimuimbia kwa utani kuwa "Abdallah Kibaden,Kanya mavi Mtendeni,kasingizia wageni" anadai jina hilo ambalo marehemu baba yake hakupendezewa nalo lakini lilishika kasi na kuzoeleka vinywani mwa watu.

Alhaj King Kibaden anasema baada ya kuendelea kuzoeleka kwa jina hilo la Abdallah Kibaden hatimaye jina lake la tatu la Seif nalo likaondoka baada ya kwenda Songea kuichezea kwa mafanikio klabu ya Maji Maji ya Songea ambapo akiwa huko licha ya kukaribishwa vizuri na wana "Lizombe" walimpatia heshima ya kipekee na walimvika jina la machifu waliokuwa katika vita ya Maji Maji alipatiwa jina la "Mputa" ambaye huyu alikuwa kiongozi wao wa katika vita ya Maji Maji hatimaye kumfanya sasa kuzoeleka kwa majina ya Abdallah Kibaden Mputa na kuachana na jina halisi la Abdallah Athuman Seif,majina haya aliyatambulisha rasmi katika mamlaka husika kama ndio yatakayotumika kama majina yake halisi.


Alhaj King Kibaden ambaye ni mmoja wa waumini wa kiislam aliyehudhuria ibada ya Hijja huko Saudi Arabia na kumfanya aitwe Alhaj anaendelea kusema kuwa yeye elimu yake ilikuwa mpaka middle school (darasa la nane) na elimu ya madrasa ya kumtukuza Mwenyezi Mungu. Anadai alipomaliza darasa la Nane alimuomba baba yake amruhusu aachane na kuendelea kielimu na badala yake ajikite kwenye soka acheze mpira wa miguu.


Alianza kucheza soka toka mwaka 1970 alipojiunga na timu ya Kahe Sports Club na kisha baadae alijiunga na timu kubwa ya wakati huo ya Sunderland ambayo kwa sasa inatambulika kama Simba SC.


Miaka nane yake ndani ya uchezaji uliotukuka katika Simba kulihitimishwa mwaka 1978 alipojiunga na "wana Lizombe" Maji Maji ya Songea. Akiwa Maji Maji alicheza mpaka mwaka 1984 kwa takriban miaka sita.Licha ya kuchezea Maji Maji lakini pia kipindi hicho alianza kusomea masomo ya "football coaching" na kuhitimu mwaka huo huo wa 1984.


Pia amesomea kozi mbalimbali za football coaching Ujerumani, Mauritius, Ubelgiji nk


Alhaj King Kibaden ana mafanikio yapi anayojivunia nayo?

Katika vitu anavyojivunia Alhaj King Kibaden ni kucheza kwa mafanikio katika Simba SC ambapo aliipa mataji kadhaa na pia kuwa na rekodi isiyosahaulika ya kufunga magoli matatu kwa mkupuo katika mechi moja ya watani wa jadi. Rekodi hiyo kwa miaka 45 sasa haijavunjwa na mchezaji yeyote katika michezo yote ya mashindano yoyote yaliyozikutanisha timu hizo kubwa Tanzania.


Pia bado ana rekodi ya kipekee ya kuipeleka Simba SC katika fainali ya michuano ya CAF ambapo akiwa Kocha mkuu wa timu ya Simba huku akisaidiwa na kocha toka Ethiopia Antenne Eshete Simba SC ilifikia Fainali ya kombe la CAF,rekodi ambayo mpaka leo miaka 29 haikuvunjwa na timu yoyote Tanzania toka kuifikia Simba mwaka huo wa 1993.


Anajivunia katika kikosi chake cha 1993 licha ya kuvifunga vilabu vikubwa vingi huku bajeti ikiwa finyu lakini alikuwa na wachezaji wote wazawa wa Tanzania waliokuwa na moyo na mapenzi ya dhati yaliyochanganyika na uzalendo kwa timu na taifa lao.


Alhaj King Kibaden pia alifundisha vilabu kadhaa vya ndani na nje ya Tanzania huku akikuza vipaji vya wachezaji wengi Tanzania.


Alhaj King Kibaden aliwahi kufundisha soka Oman na kwa hapa Tanzania alivifundisha vilabu vya Mtibwa,Simba,Maji Maji,Kagera Sugar,team za Taifa Stars na Serengeti Boys ambapo Serengeti Boys licha ya kufaulu iliondolewa katika mashindano kufuatia mchezaji Nurdin Bakari kuwa na matatizo ya "registration" yake.

Ni kipi hasa kilimpa nguvu ya kuifikisha Simba SC katika fainali ya CAF?

Akijibu swali hilo mwalimu Alhaj King Kibaden anatanabaisha kuwa maandalizi yalikuwa mazuri na kwa wakati ule team ilikuwa inasimamiwa kiufadhili na Mfanyabiashara Azim Dewji na marehemu Privatus Mtemanyenje "Priva Mtema".


Anadai kulikuwa na kambi Zanzibar ambayo ilikuwa eneo tulivu na wazanzibar walikuwa wakiisapoti kambi kwa kila kitu.


Anasisitiza kuwa imani kubwa kwa Mwenyezi Mungu iliyowashika kila aliyekuwa katika team ndio siri kubwa ya wao kufika Fainali ya CAF.


Anachokumbuka ni kuwa kila siku za swala ya Ijumaa yeye alikuwa anaomba kufanywe maombi ya timu kuwa na mafanikio.


Kingine ni motisha,anakumbuka Mfadhili Azim Dewji alikuwa anawapa motisha mbalimbali ikiwamo zawadi ya gari kwa kila mchezaji iwapo Simba itatwaa taji la CAF.Zawadi hiyo ilikuwa ni kutolewa kwa magari aina ya KIA.


Wachezaji walikuwa wanajitambua na kujituma huku yeye akiwapa elimu ya uzalendo wa taifa lao.


Alhaj King Kibaden ama kwa hakika ni nguli na mwenye kuufahamu mpira wa Tanzania na Afrika.


Anashauri klabu yake ya Simba inaweza kumtumia akatoa mchango wake kwa kuwa bado uwezo huo anao hata wa kuwa katika ushauri kwa wachezaji na benchi la ufundi.


Kwa sasa anamiliki academy yake ya soka inayofahamika kama Kibaden International Soccer Academy (KISA) iliyopo Chanika,Dar Es Salaam.


Kituo kinaendelea kuzalisha wachezaji wengi wazuri ambao wanapelekwa katika vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu na Ligi daraja la Kwanza.


Vipi kuhusu wao wachezaji wa zamani wanapewa heshima ama ushirikiano na klabu ya Simba kwa sasa?


Akijibu swali hilo Mwalimu Alhaj Kibaden anadai wanakosa ushirikiano na bila ya kuelewa sababu haswa ni nini.


Anashauri klabu iwe inawathamini wachezaji walioitetea klabu kwa kila nia na njia mpaka imepata mafanikio hapo ilipo.

Vipi kuhusu usajili?

Mwalimu Alhaj King Kibaden ametanabaisha kuwa kiutaalam hawezi kulijibu kwa kuwa mpira unachezwa kutokana na jinsi mwalimu anavyofundisha,sasa hafahamu uwezo wa Mwalimu na hata hawa wachezaji.Tofauti na zamani ambapo ulikuwa unaweza kujua uwezo wa mwalimu au mchezaji.


Ana imani kwa benchi na uongozi kuwa wanaelewa nini hasa wana Simba wanahitaji kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa,hivyo wanaweza kufanya usajili mzuri ili waonekane kuwa wamefanya kazi nzuri na kutimiza ahadi kwa wanachama,wapenzi na mashabiki wa SSC.


Ana imani wachezaji hawa wa sasa watajitahidi kwa kuzingatia kuwa sasa mpira ni ajira na wanapata sifa na pesa,hivyo si rahisi kama watafanya utovu wa nidhamu na kuwaharibia performance.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages