Breaking

Wednesday 26 October 2022

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUWAJIBIKA KATIKA KUSIMAMIA MIRADI



Na. Veronica Mwafisi-Mufindi

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kuwajibikaji kikamilifu katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ikiwemo madarasa, zahanati, vituo vya afya na miundombinu ya barabara na reli, ili fedha inayotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza miradi hiyo itumike ipasavyo kuleta maendeleo katika taifa.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo Oktoba 25, 2022 kwa watumishi wa umma nchini, wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa wilaya hiyo.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zote nchini, hivyo ni lazima tuwajibike kikamilifu katika kuisimamia miradi yote ili ikamilike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kuwajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora ili kuondoa dhana potofu iliyojengeka katika jamii kuwa, watumishi wa umma hawawajibika ipasavyo kama ilivyo katika sekta binafsi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Bw. Kenny Shilumba amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika halmashauri yake.

Naye, Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Bi. Tunu Kombo kwa niaba ya watumishi wenzie amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwapatia elimu kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.

Sanjari na hilo, Bi. Komba amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuteua viongozi mahiri wenye kujituma katika kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma nchini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza ziara ya kikazi mkoani Iringa kwa kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages