Breaking

Monday 14 November 2022

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA UBORESHWAJI MIUNDIOMBINU HIFADHI YA TAIFA KILIMANJARO




Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Mhe. Ally Juma Makoa amesema Kamati yake imeridhishwa na uboreshwaji wa miundombinu ya utalii ikiwemo barabara, njia za watalii za kutembea kwa miguu pamoja na viwanja vitakavyotumika kutua helikopta kwa ajili ya huduma za dharula katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA).

Ameyasema hayo Jumapili Novemba 13, 2022 wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua utekelezaji miradi ya fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimajaro.

“Tunaipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuboresha miundombinu katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro kwa sababu tumeweza kupanda mlima huu kwa urahisi kabisa” Mhe. Makoa amefafanua.

Mhe. Makoa amesema Kamati imeridhika na utekelezaji wa miradi hiyo na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe. Samia Suhulu Hassan kwa kuendelea kuipatia fedha Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kuhusu eneo lililokuwa linaungua kwa moto, Mhe. Makoa amewathibitishia wananchi kuwa moto huo ulishadhibitiwa na Mlima Kilimanjaro kwa sasa ni eneo salama sana na shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo ameweza kuona umuhimu wa sekta ya maliasili na utalii.

Amefafanua kuwa Kamati imeona utekelezaji wa miradi inayotokana na fedha za UVIKO 19 na imekagua njia itakayotumiwa kwa ajili ya shughuli za dharula na uokoji.

“Njia hizi mwanzoni zilikuwa zinaleta usumbufu sana na zilikua zinapelekea hata wale wageni wanaopata matatizo ya kiafya wakiwa mlimani, kuchelewa kufikishwa kwenye maeneo ya huduma mjini, lakini kwa sasa wanaweza kupatiwa huduma ya usafiri kwa haraka na kwa urahisi” Mhe. Amesisitiza Mhe. Masanja.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii inaendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Wizara ya Maliasili na Utalii mkoani Kilimanjaro.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages