Breaking

Wednesday 14 December 2022

AJALI YA BAISKELI CHANZO KIFO CHA KAPEMBE - TANAPA



Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetoa ufafanuzi juu ya taarifa ya kifo cha Joachim Vicent Kapembe raia wa Tanzania (45) kilichotokea katika Mlima Kilimanjaro.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Afisa uhifadhi mwandamizi Catherine Mbena imeeleza kuwa Kapembe amefariki dunia jana majira ya saa 12;00 jioni katika kituo cha Kibo (Kibo Hut) kufuatia ajali ya baiskeli aliyokuwa anaiendesha kama sehemu ya utalii.

Kapembe ambaye katika uhai wake alikuwa mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) alikuwa mmoja kati ya watu ambao walipanda Mlima Kilimanjaro wakati wa kwenda kuzindua mtandao wa internet katika kilele cha Uhuru.

Mwandishi huyo wa habari alifikwa na umauti wakati wa kushuka kutoka kilele cha Uhuru baada ya kupata ajali ya baiskeli aliyokuwa akiendesha kutoka kituo cha Kibo kuelekea Kituo cha Horombo. Mwili wa marehemu umehifadhi katika Hospitali ya KCMC - Moshi.

Aidha TANAPA imetoa pole kwa familia ya marehemu, watumishi wa TBC, wanahabari na Taifa kwa ujumla kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages