Breaking

Thursday 27 April 2023

BRELA KUADHIMISHA SIKU YA MILIKI UBUNIFU DUNIANI


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inaungana na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO)na nchi nyingine duniani, kuadhimisha siku ya Miliki Ubunifu ili kutoa chachu kwa wabunifu kuendelea kubuni na kuvumbua vitu mbalimbali kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 


Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za BRELA  Jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji  Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema,  maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka  ifikapo  Aprili 26, hata hivyo kwa Tanzania kwa mwaka huu yatafanyika Aprili 28, katika Kituo cha  Mikutano cha Kimataifa cha (Julius Nyerere International Convention Center -JNICC).


Bw. Nyaisa amesema lengo kuu la Maadhimisho hayo ni kutambua mchango wa Miliki Ubunifu katika maendeleo ya kijamii na  kiuchumi na kuwajengea watu ufahamu juu ya masuala ya Hataza, Hakimiliki, na Alama za Biashara na Huduma.


"BRELA itaadhimisha Siku ya Miliki Ubunifu tarehe 28 Aprili, 2023 badala ya 26 Aprili, 2023 kwa kuwa siku hiyo kwa Tanzania ni Siku kuu ya Kitaifa ya Maadhimisho ya kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kauli mbiu ya Siku ya Miliki Ubunifu mwaka huu itakuwa ni *Wanawake na Miliki Ubunifu*:*Kuongeza kasi ya Ubunifu katika Biashara", amefafanua Bw.Nyaisa


Ameongeza kuwa  siku hiyo wadau kutoka sekta za umma na binafsi watajadili  kuhusu mafanikio na changamoto za  Miliki Ubunifu   katika kukuza Biashara.


Wabunifu mbalimbali watatoa shuhuda za mafanikio na kuonesha baadhi za kazi zao za ubunifu huku  washiriki  wakikabidhiwa vyeti na tuzo kwa wabunifu mbalimbali.


Mgeni Rasmi  anatarajiwa kuwa Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages