Breaking

Saturday 28 October 2023

KILOGRAMU 6.93 ZA DHAHABU ZAKAMATWA ZIKITOROSHWA CHUNYA


Na.Wizara ya Madini - Chunya.

Madini yenye thamani ya shilingi za kitanzania zaidi ya milioni 961 yenye uzito wa kilogramu 6.93 yakamatwa wilaya ya Chunya , Mkoani Mbeya yakitoroshwa kwenda kuuzwa nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 28, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya katika machimbo ya dhahabu wilayani Chunya.

Mhe.Mavunde amesema dhahabu iliyokamatwa ina thamani zaidi ya shilingi za kitanzania milioni 961ambapo kama ingetoroshwa Serikali ingekosa mapato ya zaidi mioni 60 .


Akizungumza na wafanyabiashara wa Madini katika soko la madini Mbeya Mhe.Mavunde amewataka wafanyabiara wote wa madini kutojihusisha na njama zozote za utoroshaji madini kwani kufanya hivyo kunakosesha mapato nchini na kudumaza juhudi za kuleta maendeleo.

Aidha, Mhe .Mavunde amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ina mikakati mbalimbali ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini kwa kuwapatia mitambo ya uchorongaji , kuwajengea mazingira wezeshi ya kupata mikopo yenye riba nafuu pamoja na kufanya utafiti wa kina ili kufanya uchimbaji bila kubahatisha.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mayeka Mayeka amesema kuwa mazingira ya uchimbaji madini wilayani Chunya yanaendelea kuhimarishwa hisipokuwa changamoto kubwa ni utoroshaji madini na wizi wa Carbon katika mialo ya uchenjuaji madini.


Awali, akitoa taarifa kuhusu Sekta ya Madini Wilayani Chunya , Afisa Madini Mkazi Sabahi Nyansiri amesema mpaka sasa vituo vidogo 24 vya ununuzi wa dhahabu vimefunguliwa ili kusogeza huduma ya ununuzi na uuzaji kwa wachimbaji wadogo wasio na uwezo wa kufika katika soko kuu pamoja na wale wenye kiasi kidogo cha dhahabu.

Akielezea kuhusu mikakati kuwaendeleza wachimbaji wadogo Chunya Sabahi ameeleza kuwa kwasasa wapo na mkakati wa kurasimisha na kuboresha mfumo mzima wa uchimbaji mdogo kwa kuwatengea maeneo ya uchimbaji mdogo katika maeneo ya Godima , Isenyela na Itumbi.

Mkakati mwingine ni kufanya utafiti wa kijiolojia wa kuonesha mashapo ya miamba katika maeneo ya Itumbi, Mbigwa, Godima na Isenyela.

Katika ziara hiyo Mhe.Mavunde amekagua machimbo ya wachimbaji wadogo wa Itumbi na kufanya mkutano kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili.

Mnamo Oktoba 26 , 2023 ilitolewa taarifa kuhusu kukamatwa kwa kilogramu 6.93 za madini ya dhahabu yakisafirishwa kuuzwa nje ya nchi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages