Breaking

Wednesday 25 October 2023

SEKTA YA MADINI NGUZO MUHIMU MAENDELEO YA NCHI



Imeelezwa kuwa, Sekta ya Madini ni nguzo muhimu na chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia rasilimali madini iliyopo nchini.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 25, 2023 na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 jijini Dar es salaam.

"Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi," amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, Sekta ya Madini inafungamanishwa na Sekta nyingine za Kiuchumi kama vile viwanda na kilimo ili kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotumia madini kama malighafi mfano mbolea, betri za magari, simu, kompyuta na bidhaa nyingine.

"Niwahakikishie kuwa, mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yameendelea kuboreshwa na kuwa rafiki zaidi. Nafurahi kusema kuwa, hadi sasa jumla ya Kampuni tisa za Kimataifa za uchimbaji mkubwa wa madini zimeingia ubia na Serikali katika uchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo madini ya nikeli, kinywe, heavy mineral sands (mchanga bahari), Rare Earth Elements, dhahabu na almasi," ameongeza Dkt. Biteko

Aidha, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali inaboreshwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inanufaika na rasilimali madini, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi na Serikali inapata mapato stahiki.

"Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha kuwa mchango wake unakua hadi kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa kufikia mwaka 2025 kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Tutashirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta kuhakisha lengo hilo linafikiwa," ameongeza Waziri Mavunde.

Kwa upande mwingine, Mawaziri wa Madini kutoka nchini Malawi Mhe. Monica Chang'anamuno na Mhe.Peter Lokeres kutoka nchini Uganda wamesema kuwa Afrika ina fursa nyingi za Sekta ya Madini zinazovutia wawekezaji kuwekeza.

Mkutano wa Madini 2023 umehudhuriwa na mawaziri kutoka nje ya nchi, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Makatibu Wakuu na Manaibu Wakuu kutoa Tanzania Bara na Visiwani, Waheshimiwa Mabalozi, Viongozi wa Serikali, Vyama vya siasa na Wakuu wa Taasisi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages