Breaking

Tuesday 10 October 2023

SERIKALI YATATUA MGOGORO WA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI MAFURUNGU




Serikali kupitia Wizara ya Madini leo Oktoba 10 , 2023 imetatua rasmi mgogoro wa wachimbaji wadogo wa madini uliodumu kwa mwaka mmoja katika Kitongoji cha Mafurungu ,Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.


Akizungumza katika Mkutano na wachimbaji wadogo Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika ukuaji wa uchumi wa taifa hivyo inafanya kila juhudi ili kuona wachimbaji wadogo wa madini wapo katika mazingira salama ya uchimbaji.


Mhe.Mavunde amefafanua kuwa maana ya mazingira bora ya uchimbaji ni pamoja usalama katika uchimbaji, kuchimba kwa kutumia vifaa vya kisasa lakini pia kuwa na taarifa sahihi za uwepo wa madini ili kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.


Mavunde ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wenu katika sekta ya madini leo tunafunga rasmi mgogoro kwa kuwapatia leseni nne za uchimbaji ili kila mmoja achimbe bila kuwepo na mgogoro wowote katika kitongoji cha Mafurungu.


Sambamba na hapo Mhe.Mavunde ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji katika maeneo yao ya kazi ambapo katika juhudi za kuunga mkono maendeleo ya kitongoji cha Mafurungu tayari ametoa ahadi ya mifuko 200 ya Saruji na kuwa Balozi wa kujitolea kwa eneo hilo.


Naye, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahm Mwanga ameupongeza uongozi wa Wachimbaji Wadogo wa madini kupitia Chama Cha Wachimbaji Wadogo Mafurungu (UWAWAMA) kwa kukubali na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Madini na kuweza kufuta sintofahamu zote zilizokuwepo awali.


Awali , Meneja Mgodi Mbwana Mosses akisoma taarifa ya mafanikio ya Chama cha UWAWAMA kuhusu uzalishaji wa dhahabu amesema kuwa hadi sasa chama kupitia migodi yake kimeweza kuzalisha kiasi cha gramu 11093.19 za dhahabu ambazo zina thamani ya TZS. 1,331,419,080.67 na kulipa Mrabaha wa TZS. 79,888,144.75.


Mkutano ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo la Mvumi Livingstone Lusinde, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Afisa Madini Mkazi Dodoma,Viongozi wa Dini na wachimbaji wadogo madini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages