Breaking

Wednesday 25 October 2023

VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA KISHAPU VYAPONGEZWA MABADILIKO MAKUBWA MIAKA 30 YA TGNP

 

Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu uliofanyika leo Jumatano Oktoba 25,2023 katika kata ya Maganzo wilayani Kishapu.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Francis Philip Manyanda  akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga vimepongezwa kwa kazi nzuri vinavyoiyofanya katika jamii kuleta mabadiliko chanya hususani kufikia usawa wa kijinsia.


Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Francis Philip Manyanda wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu uliofanyika leo Jumatano Oktoba 25,2023 katika kata ya Maganzo wilayani humo kuelekea Tamasha la Jinsia 2023 linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambalo litafanyika kuanzia Novemba 7- 10,2023 katika viwanja vya TGNP Mabibo Jijini Dar es salaam.


“Mnafanya kazi nzuri, naona jinsi mnavyochochea moto kuhakikisha akina mama mnawanyanyua ili washike nafasi mbalimbali ndani ya jamii na kweli wanajitokeza sana, wameendelea kuchomoza kwenye baadhi ya maeneo”,ameeleza Manyanda ambaye ni Diwani wa Kata ya Mwadui Luhumbo.


“Nimeendelea kujifunza mambo mengi sana kwenye vituo vya taarifa na maarifa vinavyosimamiwa na TGNP kwenye hizi kata 9. Nyinyi viongozi wote mliopo kwenye vituo hivi mnajitambua sana, ukimpa hata mmoja nafasi ya kuzungumza unauona utofauti kati ya mwananchi wa kawaida na jamii hii ambayo imeelimika kwa kiwango cha juu sana”,amesema Manyanda.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Francis Philip Manyanda.

“Kwanza mmepata bahati ya pekee kufundishwa namna ya kujiamini, namna ya kukaa na watu, namna ya kukaa kwenye mikutano ya hadhara lakini namna ya kupangilia nianzie wapi kuzungumza, nikomee wapi. Tumeendelea kujivunia sana uwepo wenu ndani ya wilaya yetu, jinsi mnavyoelimisha jamii",amesema.

Aidha amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kufikia usawa wa kijinsia kwa asilimia 50 kwa 50.


“50 kwa 50 haitatokea kama nyinyi wenye hamtaamua kwa dhati kugombea nafasi za uongozi, endeleeni kushikamana na kupendana na muwe na uthubutu wa kushika nafasi za uongozi, mfano mwaka 2024 tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni matumaini yangu mtajitokeza kwa wingi, naomba wanawake msikate tamaa”,ameongeza Makamu Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Diwani kata ya Maganzo Mbalu Kidiga amevipongeza vituo vya taarifa na maarifa kwa kazi nzuri wanayofanya katika jamii.

“Unajua kazi yoyote ni ushirikishwaji, ninawapenda kwa sababu mnakaa kwa kushirikiana, mnaheshimiana na mnapendana na ndiyo maana kazi zenu zinaonekana. Sisi tuko nyuma yenu na tuko tayari kuwapa ushirikiano wakati wowote, sehemu yoyote mtakayokwama msisite kutushirikisha.

“Kwa kweli mmepiga kazi sana kwenye hizi kata zetu, wanawake mnachapa kazi na sasa nchi inaongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mwanamke anayechapa kazi vizuri na nyinyi endeleeni kuchapa kazi ili tuifikia 50 kwa 50. Wanawake mnaweza”,ameongeza Diwani huyo wa kata ya Maganzo ambayo pia ina kituo cha taarifa na maarifa.


“TGNP inafanya kazi kwenye kata 9, kata zingine zinatamani na wao wapate vituo vya taarifa na maarifa, tunaamini vituo vitaendelea kuongezwa”,ameongeza Kidiga.


Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum Kishapu, Mhe. Felister Boniphace Yahula ambaye  ni zao la kituo cha Taarifa na Maarifa baada ya kujengewa uwezo na TGNP amesema anajivunia vituo vya taarifa na maarifa kwani vimembadilisha kifikra na uwezo wa kusimama mbele ya jamii kuzungumza na hatimaye kushika nafasi hiyo ya uongozi.


“Nawaasa akina mama tusikate tamaa, tuwe wajasiri, kujiamini, kuthubutu hii itatufikisha mbali. Tuendelee kushirikiana na kupendana, vituo hivi vya taarifa na maarifa vimenifanya nifike hapa nilipo, nijiamini na kushika nafasi hii ya uongozi…Mimi sikuwa na uwezo wa kusimama na kuzungumza mbele za watu. Ninawashukuru sana TGNP kwa kuanzisha vituo vya taarifa na maarifa, vinatuinua sana sisi akina mama, sisi tunaibua changamoto za jamii, serikali inaona na inachukua hatua”,amesema Felister.


“Mwakani 2024 kuna uchaguzi wa serikali za mitaa kuna uchaguzi lakini pia mwaka 2025 kuna uchaguzi Mkuu, tusiwaogope wanaume, tujitokeze kugombea ili tufikie 50/50. Tusikate tamaa, zinapotokea nafasi za uongozi tujitokeze kugombea nafasi za uongozi”,ameongeza.

Naye Diwani wa kata ya Bunambiyu, Mpemba Juma amesema vituo vya taarifa na maarifa vimekuwa na msaada mkubwa katika jamii na kwamba ushirikiano uliopo ni mkubwa kwani pia wanashirikisha pia kwenye vikao vya maendeleo ya kata.

Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo amesema wanaposherehekea miaka 30 ya TGNP, wanajivunia mafanikio kadha wa kadha wilayani humo.


"Tangu kuanzishwa kwa vituo vya taarifa na maarifa wilayani Kishapu mwaka 2012, tunayo mafanikio makubwa ya kujivunia mfano kwenye sekta ya elimu katika kata zenye vituo vya taarifa na maarifa kuna ongezeko la matundu ya vyoo shuleni, miundombinu inayojengwa shuleni inalenga makundi yote, vyumba vya usiri kwa wanafunzi wa kike, halmashauri kutenga bajeti kwa ajili taulo za kike kwa wanafunzi, walimu wa kike wameongezeka, huduma ya maji ipo kwenye baadhi ya shule, kuna ongezeko kubwa la vyumba vya madarasa, madawati, utoro shuleni umepungua, watoto wa kike sasa wanasoma, mimba na ndoa za utotoni zimepungua, tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan",amesema Madundo.
Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa wilaya ya Kishapu, Rahel Madundo.

Upande wa Sekta ya Afya, zahanati zinaendelea kujengwa na huduma muhimu zinawekwa na upande wa huduma za maji changamoto inaendelea kupungua kutokana na serikali na wadau kuendelea kuchukua hatua, hata hivyo changamoto ya maji bado ni kubwa licha ya kwamba maeneo mengi bajeti imetengwa na Serikali na huduma za wananchi kupelekewa huduma za umeme zinaendelea.


Kuhusu ukatili wa kijinsia, mabadiliko ni makubwa ambapo sasa jamii imeamka sana na inatoa taarifa kuhusu matukio ya ukatili wa kijinsia baada ya kupata elimu, hali ambayo imechangiwa sana na vituo vya taarifa na maarifa kulipigia kelele sana.


“Wakati tunaanza hizi harakati suala la ukatili wa kijinsia lilikuwa kali sana, hivi sasa matukio yamepungua, linazidi kumomonyoka siku hadi siku, tunaishukuru sana TGNP kwa kutupatia elimu ya kupambana na ukatili katika jamii. Hivi sasa wanawake wengi wameingia kwenye nafasi za uongozi ambapo wanawake wengi wameweza kutambuliwa na kuingizwa kwenye uongozi, sasa wanawake wanashiriki kwenye ngazi za maamuzi”,ameongeza Madundo.
Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Mkoa wa Shinyanga, Fredina Said.

Kuhusu masuala ya kilimo hivi sasa wanawake wanashirikishwa kwenye kilimo tofauti na mwanzo.

Katibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Kishapu, Peter Nestory amesema kazi ya Vituo vya taarifa na maarifa ni kuibua changamoto na kuihamasisha jamii kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.

Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Mkoa wa Shinyanga Fredina Said ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kuchukua hatua madhubuti inazochukua katika kumpigania mwanamke ikiwemo kutenga Bajeti kwa mrengo wa Jinsia, ambapo ameishukuru Halmashauri hiyo kwa namna inavyoshirikiana na vituo vya taarifa na maarifa katika kutatua changamoto za jamii.


Pia ameviomba vituo vya taarifa na maarifa jamii kutoa elimu kwa jamii kuhusu Mikopo inayotolewa katika jamii ili iepukane na mikopo umiza ambayo inawaathiri sana wanawake kiuchumi.

Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Maganzo, Neema Gwesso akizungumza kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Kishapu amesema vituo vya taarifa na maarifa vimekuwa chachu ya maendeleo hivyo kuwataka wadumishe nidhamu, upendo na mshikamano ili kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika jamii kwani kazi zao ni nzuri na zinaonekana.


Aidha amewataka wanawake kuchangamkia fursa ya mikopo bila riba inayotolewa katika Halmashauri na wawe waaminifu kurudisha kwa wakati.
Wakiwasilisha taarifa za vituo za taarifa na maarifa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012, wanachama wa vituo hivyo wameishukuru TGNP kwa kuwapa mafunzo ya kuiwezesha jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.

Aidha wamesema wanaposherehekea miaka 30 ya TGNP wameeleza kuwa hivi sasa Wanawake wanajitambua vizuri na watoto wa kike wamejitambua hali iliyochangia kupungua kwa mimba na ndoa za utotoni.

“Elimu iliyotolewa na TGNP imeleta mabadiliko makubwa ya kuonekana kabisa siyo maneno maneno tu. Wanawake wamebadilika wanaomba uongozi nafasi mbalimbali. Mabadiliko ni makubwa tumejitambua sana”,wameongeza.

Wamezitaja changamoto zilizopo sasa bei ndogo kwenye zao la pamba,choroko hali inayodumaza uchumi.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Francis Philip Manyanda  akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu uliofanyika leo Jumatano Oktoba 25,2023 katika kata ya Maganzo wilayani Kishapu. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Diwani kata ya Maganzo Mbalu Kidiga akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu.
 Mratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Mkoa wa Shinyanga, Fredina Said akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu.
Katibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilaya ya Kishapu, Peter Nestory akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu.
Diwani wa kata ya Bunambiyu, Mpemba Juma akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu.
Diwani wa Viti Maalum Kishapu, Mhe. Felister Boniphace Yahula akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu

Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Maganzo Neema Gwesso  kwa akizungumza kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Kishapu wakati wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu
Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu ukiendelea
Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu ukiendelea
Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu ukiendelea
Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu ukiendelea
Washiriki wa Mkutano wa Baraza la Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu wakipiga picha ya kumbukumbu,

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages