Breaking

Wednesday 25 October 2023

WAZIRI DKT.SAADA AZINDUA KAMPUNI YA AIRPAY

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na mipango Zanzibar Dk. Saada Mkuya Salum, amesema kuwa uamuzi wa kampuni ya Airpay kuanzisha kituo cha teknolojia nchini utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampuni hiyo ya AirPay Tanzania ulioenda sambamba uzinduzi wa mtandao wa idara ya mashirikiano baina ya serikali na sekta binafsi(PPP), amesema mfumo huo utakuza uchumi wa nchi hasa ikizingatiwa kuwa serikali ya Zanzibar inatekeleza sera za uchumi wa bluu na inajitahidi kuweka mazingira mazuri ili kuvutia wawekezaji.

Akizungumzia ajenda ya mifumo ya digitali nchini, waziri huyo alitoa rai kwa taasisi mbalimbali za serikali kutumia mifumo ya wakala wa serikali mtandao na kuitaka taasisi hiyo kuhakikisha usalama wa mifumo inayoanzishwa ili kupunguza changamoto za kifedha.

Aidha aliishauri kuzisaidia taasisi na mashirika ya umma kuyafikia masoko ya kidigitali ili kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo kujenga utamaduni wa matumizi ya mifumo ya malipo kidigitali badala ya fedha taslimu.

“Pongezi na shukrani kwa serikali ya India kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar na Tanzania jambo linalokwenda kuimarisha zaidi uhusiano mzuri”amesema.

Amesema kipindi kirefu serikali ya Zanzibar ikijaribu kutafuta suluhisho kutoka katika matumizi ya fedha taslim na kwenda kulipia kimtandao ambao hakuna sababu ya kubeba fedha kwa ajili ya kununua bidhaa au kufanya malipo mbalimbali.

Amesema pia ni fursa kwa wajasiria mali kutambulika na kuweza kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha.

Waziri wa nchi, ofisi ya rais, kazi, uchumi na uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga amesema kuwa mfumo wa malipo uliozinduliwa utachangia ukuaji wa uchumi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Ameeleza kuwa mfumo huo unajumuisha makundi yote yanayohusika na biashara, ujasiriamali na uhaulishaji wa fedha na mfumo huo sio mgeni na nchi mbalimbali unatumia na lengo mahsusi serikali kuwa na takwimu halisi ya mwenendo wa uchumi.

“Katika mazingira yetu ya Zanzibar zaidi ya asilimia 70 ya wafanyabiashara bado hawajarasimishwa hivyo hakuna takwimu halisi za uchagiaji wa kodi kwa wafanyabiashara hao wakiwemo wakubwa, wakati na wadogo”amesema Soraga.

Waziri wa biashara na viwanda Omar Said Shabani, alisema mfumo huo wa air pay utawezesha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara katika kufanya malipo lakini si kwa wafanyabiashara pekee hata watoa huduma.

Amesema mfumo huo utaleta mapinduzi makubwa katika mazingira mazuri ya biashara, ufanyaji wa malipo na mambo mingine na wizara yake inatarajia kufanya maonesho ya kibiashara hivyo mfumo huo utumike katika ulipaji ambapo huduma hiyo ni salama.

Kamisha wa Idara ya Mashirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) Dk. Bili Kiwia, amesema mfumo huo wa air pay utasaidia kurasimisha wajasiriamali, sekta isiyo rasmini kufanya biashara kidigitali pasipo na uhitaji wa fedha taslim.

Naye Mwazilishi mweza wa Airpay Tanzania Yasmin Chali, amesema wameamua kuwekeza Zanzibar kutokana na umahiri wake kwenye biashara na uvumbuzi wa masuala mbali mbali hivyo watajitahidi kuhakikisha uwekezaji wao unawanufaisha watu wote.

Ameeleza kuwa katika kufuikia lengo hilo watahakikisha wanatoa elimu ya matumizi jumuishi ya fedha ili kuwafanya wajasiriamali na watumiaji wengine wa huduma za kifedha kukua kibiashara lakini pia kupata suluhu juu ya masuala ya fedha.

Kwa upande wake Mwanzilishi wa Kampuni ya Airpay, Kunal Jhunjhunwala alisema " Lengo letu tunataka kumfikia mtuwa kawaida kabisa na kwa jinsi Zanzibar inavyoendelea tumeona ni mahali sahihi kuja kuwekeza, tunataka kutoa huduma bora katika nchi zaidi ya 12," amesema

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages