Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Serikali imesema Mfumo Unganishi wa Kutunza Taarifa za Ardhi unaoboreshwa na timu ya wataalamu jijini Arusha utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto mbalimbali za sekta ya ardhi nchini.
Mfumo huo unaotarajiwa kuanza katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Tanga utarahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma za sekta ya ardhi kwa kuwa wananchi watakuwa wakipata huduma kwa njia ya mtandao.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda mkoani Arusha tarehe 22 Novemba 2023 alipokutana na kuzungumza na Menejiment ya Wizara pamoja na Timu ya wataalamu inayooboresha Mfumo huo.
Amesema, sekta ya ardhi imekuwa na changamoto nyingi lakini hatua ya wizara ya Ardhi kufanya maboresho ya kimfumo kutasaidia kuondoa kero na kelele za wananchi kwenye masuala ya ardhi.
‘’Kikubwa ambacho nimeanza kufarijika ni kwamba ‘mmeadvance’ mpaka hapa mlipofika katika kuboresha mfumo, hongereni sana baada ya muda tutakwenda kumaliza kelele za wananchi wa nchi hii’’ alisema Mhe. Pinda.
Kupitia maboresho ya mfumo huo unganishi wa kutunza taarifa za ardhi changamoto zote za sekta ya ardhi ikiwemo upatikanaji namba ya malipo, malipo ya ada mbalimbali, upatikanaji hati, uthamini pamoja na migogoro ya ardhi zinaenda kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya kimtandao.
Kwa mujibu wa Pinda, itachukua muda kufikia malengo yaliyokusudia katika kuboresha mfumo huo kwa sababu kinachofanyika sasa ni kuwahamisha wananchi kutoka kwenye mfumo waliouzoea na kwenda katika teknolojia mpya.
Hata hivyo, amewatahadharisha wataalamu wanaoboresha mfumo huo pamoja na maofisa wa wizara ya ardhi kuwa makini kutokana na upinzani wanaoweza kuupata kutoka kwa baadhi ya watu aliowaeleza kuwa ni wanufaika wa mifumo ya sasa ambayo wizara ya ardhi inaenda kuachana nayo.
‘’lazima mkawe standby wakurugenzi na maofisa, wale waliokuwa wanakula kupitia mfumo wa kawaida mjue ndiyo ‘threat’ namba moja wao ndiyo watakaoanza kusema mfumo wa ardhi bure kabisa lazima tutengeneze timu ya kuwaattack’’ alisema Pinda.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera alimueleza Mhe. Pinda kuwa, Menejiment ya wizara imepitia kila hatua ya jinsi mfumo unavyofanya kazi lengo likiwa kufanya maboresho yatakayowezesha idara za wizara hiyo kutekeleza majukumu kwa ufanisi.
‘’Kupitia mawasilisho ya wataalamu tungetamani mfumo ukamilike mapema lakini kwa kuwa kazi hiyo inahitaji utaalamu, tunaamini kazi hiyo itakamilika ndani ya muda mfupi’’ alisema Lucy
Mkurugenzi wa Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Ardhi Bw. Flateny Michael Hassan alisema, kufutia wizara ya ardhi kuwa na changamoto kadhaa kwenye mifumo yake imeonekana upo uhitaji wa kuunganisha mifumo yote ili kuwa na mfumo mmoja utakaohusika na sekta ya ardhi.
Amebainisha kuwa, kazi inayofanyika ya kuboresha mfumo kwa sasa imefikia asilimia 75 na ni matarajio yake mapema Januari 2023 mfumo utaanza kutumika katika mkoa wa Arusha kabla ya kuendelea na mikoa mingine.
Ameyataja maboresho yanayoendelea kufanyika kuwa ni pamoja na mfumo unaoruhusu watumishi wa sekta ya ardhi kutekeleza majukumu yao ndani ya ofisi zao, mfumo unaoruhusu wananchi kuomba huduma kwa njia ya mtandao na huduma ya Mobile App ambapo mwananchi anaweza kupata huduma kupitia simu ya kiganjani.
‘’Katika maboresho yanayoendelea, kuna mifumo mitatu wa kwanza ni Back Office unaoruhusu watumishi kutekeleza majukumu yao ndani ya ofisi, wa pili ni Public Portal unaoruhusu wananchi kuomba huduma online na wa tatu ni Mobile App ambapo wananchi wanaomba huduma kupitia simu janja’’ alisema Flateny.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa katika jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma za sekta ya ardhi zinapatikana kwa urahisi na haraka na uboreshaji mfumo huo pamoja na uwepo wa Klinik za Ardhi ni sehemu jitihada hizo ambazo zinaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wananchi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akizungumza na Menejiment ya Wizara pamoja na Timu ya wataalamu wanaoboresha Mfumo Unganishi wa Kutunza Taarifa za Ardhi jijini Arusha tarehe 22 Novemba 2023. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera.
Sehemu ya Menejiment ya Wizara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda (Hayupo pichani).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera akizungumza wakati Naibu Waziri Mhe. Geofrey Pinda alipokutana na Menejiment na Timu ya wataalamu wanaoboresha Mfumo Unganishi wa Kutunza Taarifa za Ardhi jijini Arusha tarehe 22 Novemba 2023.
Menejiment na timu ya wataalamu wanaoboresha Mfumo Unganishi wa Kutunza Taarifa za Ardhi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Geofrey Pinda (haupo pichani) alipokutana nao jijini Arusha tarehe 22 Novemba 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)