Breaking

Thursday 23 November 2023

TUWE WAZALENDO NA MIRADI YETU- MHE.MAJALIWA

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amezitaka Taasisi na Mashirika ya Umma kote nchini yanayotekeleza miradi mbalimbali kuwa na uzalendo na kuweka mbele maslahi ya taifa.

Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo ikiwa ni matokeo ya kutekelezwa kwa weledi,ufanisi, kiwango na uzalendo mkubwa kwa Mradi wa Maji wa Itumba-Isongole wilayani Ileje,mkoa wa Songwe,ambapo Leo tarehe 23 Novemba, 2023 ameweka jiwe la msingi la mradi huo.

Mhe. Waziri Mkuu amempongeza Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ((Mb na Naibu wake , Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) pamoja na wataalamu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa usimamizi mzuri wa fedha za mradi wa maji wa Itumba -Isongole na kutekeleza mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6 kati ya bilioni 4.9 ambazo zilitengwa ili kutekeleza mradi huo,hivyo kubaki kwa fedha ya serikali ambayo itatekeleza miradi mingine ya maji, na kwamba ni vema watekelezaji wa miradi ya serikali wakajenga utamaduni wa uzalendo na uadilifu katika matumizi ya fedha za umma.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Mary Prisca Mahundi (Mb) amemuwakilisha Waziri wa Maji, katika ziara hiyo ya siku nne ya Mhe. Waziri Mkuu,mkoani Songwe kuanzia tarehe 22 -25 Novemba, 2023.

Mhe. Godfrey Kasekenya, Mbunge wa Jimbo la Ileje ameipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa mradi wa maji wa Itumba-Isongole ambao utaondoa kabisa tatizo la hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 100 wilayani Ileje na kuwa na ziada ya maji.

Mradi wa Maji wa Itumba-Isongole katika Wilaya ya Ileje,mkoani Songwe unatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji ( NWF) na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba 2023 na utahudumia wananchi zaidi ya elfu ishirini wa miji ya Itumba na Isongole wilayani Ileje.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages