Breaking

Wednesday 7 February 2024

COCO BEACH WAFUNGULIWA KITUO CHA HUDUMA KWA UMMA

Wafanyabiashara wa eneo la Coco beach pamoja na wnaufaika wa mradi wa vituo vya huduma kwa jamii wametakiwa kuwa waangalifu na waaminifu katika kulinda na kutunza miundombinu ya mradi wa vituo vya kutoa huduma kwa jamii ili huduma iwe endelevu na bora kwa wote.

Hayo yameelezwa na Msimamizi wa Miradi ya Uboreshaji Usafi wa Mazingira Ndugu Charles Makoye mara baada ya uzinduzi wa kituo hicho kilichopo Coco beach, Wilaya ya Kinondoni ambacho ni sehemu ya vituo 30 vilivyojengwa na Serikali kupitia DAWASA.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka imejenga vituo hivi vya kutolea huduma kwa lengo la kuboresha Usafi wa Mazingira kwenye maeneo yote ya biashara na ya makazi.

“Huu ni mradi wa mfano na wa kisasa ambao umejengwa mahususi kwa lengo la kukabiliana na uchafuzi wa mazingira pamoja na kuweka mazingira safi kwa afya ya kila mmoja, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuulinda mradi huu ili uwe na tija kwa sasa na kwa baadae,” amesema.

Ameongeza kuwa mradi umezingatia utoaji wa huduma kwa makundi yote ikiwemo watu wenye changamoto ya viungo (walemavu).

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara eneo la Coco Beach Mussa Miamba ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuona uhitaji mkubwa wa huduma hizi na kujenga mradi huu, tunaamini mradi huu utatunufaisha sote kwa kuwa wahitaji ni wengi eneo hili.

Amewaasa wafanyabiashara wa eneo hilo kuwa waaminifu katika kutumia huduma hii kwa kutunza na kulinda miundombinu yote iliyopo ili mradi huu uwe wa muda mrefu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao wameelezea umuhimu wa vituo hivyo vya kutolea huduma na kusema kuwa mradi umetekelezwa kwa wakati muafaka kwani uhitaji wa huduma ya namna hii ni mkubwa kwa watu wote.

Rashid Mfaume mfanyabiashara wa chakula na vinywaji amesema kuwa kukosekana kwa huduma ya choo kwenye maeneo yao ya biashara kumeleta athari kwa muda mrefu hususani kwenye biashara za chakula

“Hapo awali ilikuwa ngumu kupata wateja wa chakula na vinywaji kwa uhuru kwa kuwa hamna huduma ya maliwato kwenye eneo hili, hivyo tumekosa wateja wengi. Hii kwetu ni fursa ya kipekee ya kuboresha mazingira ya biashara. Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kuweka huduma hii kwenye maeneo haya, ni hatua nzuri ambayo itasaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko,” ameeleza.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages