Breaking

Tuesday 26 March 2024

AMEND WAELEZEA SABABU ZA KUTOA MAFUNZO YA HUDUMA YA KWANZA KWA MADEREVA BODABODA TANGA

Na Mwandishi Wetu,Tanga

TAASISI ya AMEND inayojihusisha na utoaji wa elimu ya usalama barabarani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo yenye shule wameeleza sababu za kutoa elimu ya huduma kwanza kwa madereva bodaboda mkoani Tanga.

AMEND wamekuwa wakitoa elimu ya usalama barabarani pamoja na mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva hao kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania lengo likiwa kupunguza ajali za barabarani kwa kundi hilo ambalo kwa sehemu kubwa limekuwa likiathirika zaidi na ajili za barabarani.

Wakizungumza Kuhusu elimu inayotolewa na AMEND kwa ufadhili wa Uswisi,baadhi ya wadau wameelesa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa madereva bodaboda katika Jiji la Tanga.

Akizungumza kuhusu mradi huo,Ofisa Miradi kutoka taasisi ya AMEND Scolastica Mbilinyi amefafanua lengo la kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa bodaboda ni kusaidia kuokoa maisha ya watu pindi ajali zinapotokea.

"AMEND miongozi mwa mambo tunayofanya ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani, ujenzi wa miundombinu ya barabara kwenye shule zilizopo maeneo hatarishi na kwa wakati huu huo tunatoa elimu ya huduma ya kwanza kwa madereva kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wakati wa ajali,"amesema Mbilinyi.

Kwa upande wake CPL Hamisi kutoka Ktengo cha Elimu kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga akizungumzia umuhimu wa huduma ya kwanza pale ajali inapotokea, amesema ni sahihi kwa mtu aliyepata elimu ya huduma ya kwanza kutoa huduma kwa mtu aliyepata ajali.

Amesema kwa kufanya hivyo kunasaidia kuokoa maisha pamoja na kukisaidia jeshi la polisi katika utekelezaji wa majukumu yake huku akitoa rai kwa baadhi ya bodaboda kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu zinapotokea ajali.

"Ni vema madereva bodaboda ambao mmepata elimu hii ya usalama barabarani pamoja na elimu ya kutoa huduma ya kwanza mkawa mstari wa mbele katika kusaidia jamii pindi inapotokea ajili katika maeneo mtakayokuwepo.Acheni kujihusisha na vitendo vya uhalifu,najua sio wote wenye tabia hiyo,ila wale wanaojihusisha na uhalifu waache."

Amesisitiza kuwa ni muhimu watumie elimu waliyoipata kuokoa maisha ya waliopatwa na ajali barabarani.

Wakati huo huo Diana Kashmiry kutoka katika Kikosi kazi cha huduma ya kwanza kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu amesema elimu wanayoitoa inamuwezesha dereva bodaboda kujua changamoto aliyoipata mtu katika ajali na namna bora ya kumsaidia kwa kumpa huduma ya kwanza

Amesema kutokana na mazingira hatarishi yanayokuwepo kwenye ajali, ametoa mwito kwa mtu ambae hana vifaa vya huduma kwanza kutofanya zoezi kwa ajili ya kujilinda na athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo kupata magonjwa ya kuambukiza.

Shirika la AMEND kwa ufadhili wa ubalozi wa Uswiswi wamendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa bodaboda wa mikoa ya Dodoma na Tanga huku lengo likiwa ni kuwafikia bodaboda 750 kwenye mikoa hiyo ili kupungua ajali zilizopo pamoja na kupunguza athari zinazotokana na ajali hizo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages