Breaking

Thursday 7 March 2024

THE UNIVERSE: MAAJABU YA DUNIA YALIYOJIFICHA



Na Samir Salum, Lango La Habari

Dunia, sayari yetu ya nyumbani, ni ulimwengu usiofanana na mwingine wowote. Sayari ya tatu kutoka kwa jua, Dunia ni mahali pekee katika ulimwengu unaojulikana ambao umethibitishwa kuwa mwenyeji wa maisha.

 Ikiwa na ukubwa wa maili 3,959, Dunia ni sayari ya tano kwa ukubwa katika mfumo wetu wa jua, na ndiyo pekee inayojulikana kwa uhakika kuwa na maji ya kioevu kwenye uso wake.

Dunia yetu ina siri nyingi zilizofunikwa na mjadala wa kila siku. Hapa tutachunguza baadhi ya ukweli usiojulikana mara nyingi kuhusu sayari yetu, Nyumba yetu ya Pamoja.

-Umri wa Dunia

Mnamo mwaka 1862 Mwanafizikia na mwanahisabati maarufu wa Ireland, Lord Kelvin akitumia njia ya upimaji wa joto la dunia akidhani kwamba dunia ilkuwa ikiongezeka joto polepole, hivyo alipima joto la dunia na kuangalia jinsi joto linavyopungua, na kukadiria kuwa Dunia ina umri wa miaka milioni 20 hadi milioni 400.

Lakini makadirio yake, yalipingwa na wanasayansi wengi na kuonekana dhaifu kwani mbinu yake haikuzingatia michakato mingine muhimu ya kijiolojia.

Kutokana na kuendelea kwa teknolojia wanasayansi waliendelea kufanya chunguzi mbalimbali ambapo njia ya kuchunguza miamba, vimondo, na mawe kutoka mwezini,kwa kutumia radiometric dating yaani njia ya kubainisha umri wa kitu kwa kuvunjika miamba au halijoto ya madini kutumia vifaa kama vile spectrometa ya thermal ionization mass.

Data zote kutoka Duniani na kwingineko zimeonesha Dunia inakadiriwa kuwa na umri wa miaka bilioni 4.6 kwa upungufu ama ongezeko la miaka Milioni 50.

Makadirio hayo yanatokana na tafiti za miamba ambapo wanasayansi wamegundua miamba kongwe zaidi duniani ikiwemo miamba ya Acasta Gneiss iliyopo Karibu na Ziwa kuu la Slave Kaskazini-Magharibi mwa nchi ya Canada ambayo ina umri wa miaka bilioni 4.03

Pia nchini Australia wanasayansi waligundua madini yenye umri wa miaka bilioni 4.3, hivyo kuifanya sayari ya 3 kutoka lilipo jua kuwa na umri wa miaka bilioni 4.6.

-Umbo la dunia

Dunia sio tambarare, lakini sio duara pia, dunia ina umbo la oblate spheroid, ikiwa na maana kuwa ni duara lililojifinya kidogo kwenye kingo zake na kuifanya kuwa sio duara kamili.

kupitia shilinga la anga za juu la ulaya (ESA) linaeleza kuwa sababu ya mzunguuko wa dunia inafanya dunia kuwa na uvimbe kwa katikati na kuwa tambarare kwenye kingo Za juu na chini ambapo uzito kwenye dunia una sababisha mvutano Kwenye sehemu tofauti tofauti ya sayari.

Tofauti hizi ni ndogo sana kiasi kwamba huwezi kuziona na kufanya dunia kuonekana duara kwa macho ya kawaida lakini kiuhalisia sio duara kamili. kwa urahisi tunaweza kusema dunia ina umbo la yai.

Hata hivyo wapo wanaosema kuwa dunia ni tambarare lakini bado hawana uthibitisho wa moja kwa moja na mijadara mirefu bado inaendelea juu ya umbo halisi la dunia.

-Urefu wa siku ya Dunia unaongezeka.

Wakati Dunia iliundwa miaka bilioni 4.6 iliyopita, siku yake ilikuwa na urefu wa takriban masaa sita. Kufikia miaka milioni 620 iliyopita, urefu wa siku uliongezeka hadi saa 21.9. Leo, wastani wa siku ni urefu wa saa 24, huku wanasayansi wakieleza kuwa urefu wa siku unaongezeka kwa takriban milisekunde 1.7 kila karne.

Cha kushangaza ni kuwa mnamo tarehe 19 mwezi wa 7, 2020 dunia ilimaliza mzunguuko wake kabla ya masaa 24 kwa milisekunde 1.47 ambapo tena ilijirudia mwaka 2022 tarehe 29, mwezi wa 7 ambapo dunia ilimaliza mzunguuko wake kabla ya masaa 24 kwa milisekunde 1.59 na hakuna anaejuwa sababu japo wanasayansi wamejaribu kuelezea kuwa yawezekana ikawa ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.

- Dunia ina miezi miwili?

Yawezekana wengi tunafahamu kuwa dunia jirani yake wa karibu ni Mwezi ulio umbali wa zaidi ya kilomita laki 3,

Kupitia Shirika la anga za juu la Marekani (NASA) limeeleza kuwa mnamo Mwaka Oktoba 10, 1986 Duncan Waldron kwa kutumia picha za telescope ya Schmidt ya Uingereza iliyopo nchini Australia aligundua uwepo wa kitu kikubwa angani kinachozunguuka karibu na dunia.

Baadae kitu hicho kiligundulika kuwa ni asteroid yaani mwamba mkubwa na kilipewa jina la 3753 Cruithne, asteroid hii ina ukubwa unakadiriwa kuwa na kilomita 5 kwa upana ikiwa umbali wa kilomita milioni 12 mara tatu ya umbali wa dunia na jua.

Mwamba huu kubwa hulizunguka jua kwa mwaka mmoja kama Dunia, cha kushangaza ni kuwa jiwe hili kubwa badala ya kuzunguuka jua kwa mzunguuko wa duara, hutumia mzuunguuko wa mfano wa umbo la maharagwe au kiatu cha farasi na huchukua takribani miaka 770 kuumaliza mzunguuko huo na hii iligundulika mwaka 1997 na wanaastonomia katika chuo cha Queen Mary na westfield London.

kutokana na uwepo wa Mwamba huo wengi wameupa jina la mwezi wa pili wa dunia, japo jina hilo haliendani na uhalisia kutokana na udogo wake kwani mwezi una ukubwa wa kilometa 3475

- Mlima Everest sio Mrefu Mauna kea ndio mrefu

Mlima Everest uliopo katika safu za himalaya kwenye mpaka kati ya Nepal na China mara nyingi hutambuliwa kuwa mlima mrefu zaidi duniani ukiwa na urefu wa mita 8849 sawa na futi 29,035. lakini ukweli ni kuwa upo mlima mrefu zaidi ya everest, mlima huo unaitwa Mauna Kea, mlima huu unapatikana katika Visiwa vya Hawai nchini Marekani.

unapopima kutoka kwenye msingi hadi kileleni, Mauna Kea ina urefu wa futi 33,500 sawa na mita 10210, huku Mlima Everest ukiwa na urefu wa futi 29,035 pekee sawa na mita 8849. Hata hivyo, Mlima Everest ni mrefu kuliko Mauna Kea unapopimwa kutoka usawa wa bahari na kwa sababu everest imekaa juu ya ardhi huku Mauna Kea ukiwa kwenye kisiwa kilicho katikati ya Bahari ya Pasifiki.

Everest ikiwa na futi 29,035 juu ya usawa wa bahari. Mauna Kea inasimama futi 13,796 sawa na mita 4205 juu ya usawa wa bahari, lakini mlima huo una urefu wa futi 19,700 sawa na mita 6004 chini ya Bahari ya Pasifiki. Zaidi ya nusu yake imezama.

Mauna Kea ni volkano isiyofanya kazi yenye umri wa takriban miaka milioni moja na Ililipuka mara ya mwisho kama miaka 4,600 iliyopita.

-Jangwa la Atacama sehemu kame zaidi duniani

maeneo mengi yenye majangwa huwa na ukame, lakini Jangwa la Atacama lililoko Amerika Kusini kaskazini mwa nchi ya Chile linazingatiwa sana kuwa mahali pakame zaidi Duniani.

Eneo hili kubwa la ardhi linachukua zaidi ya kilomita za mraba 100,000 na hupokea wastani wa chini ya 1 mm ya mvua kwa mwaka.Inaaminika kwamba mji wa Atacama wa Calama haukupata mvua kwa miaka 400 . Tofauti na jangwa nyingi, Atacama ina baridi kiasi .

Wanasayansi wa NASA husafiri hadi Atacama ili kutafuta vijidudu wanaoishi katika mazingira magumu sana, wakitumaini kujifunza jinsi maisha yanaweza kuwepo kwenye sayari nyingine.

- Maajabu ya Bara la Antaktika

Huenda haishangazi kwamba mahali penye baridi zaidi Duniani ni katika Bara la Antaktika lililopo kusini mwa dunia na lenye ukubwa wa kilometa za mraba milioni 14, lakini naomba nkujuze kuwa Kulingana na Jumba la Makumbusho la Marekani la Historia ya Asili limeeleza kuwa sehemu ya barafu ya Antaktika ina asilimia 70 ya maji safi ya Dunia na asilimia 90 hivi ya barafu yake, ingawa ni bara la tano kwa ukubwa.

Je! unajua Antaktika inachukuliwa kuwa jangwa? Maeneo ya ndani hupata tu inchi 2 (milimita 50) za mvua kwa mwaka (kawaida kama theluji, bila shaka).

-Eneo lenye joto zaidi duniani

Mnamo Julai 1913, watafiti katika eneo la Furnace Creek, California sehemu ijulikanayo kama Death Valley, walitazama kipimajoto ambacho kilionesha kufikia nyuzi joto 134 (56.7°C) na kutangaza kuwa ndicho joto la juu zaidi kuwahi kurekodiwa Duniani. 

Lakini miaka tisa tu baadaye, mnamo Septemba 13, 1922, kituo cha hali ya hewa huko El Azizia, Libya, kilirekodi halijoto ya nyuzi joto 136.4 (58.0°C Selsiasi) Kulingana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), hilo linasalia kuwa joto la juu zaidi la hewa kuwahi kupimwa.

kulingana na NASA Earth Observatory kuna uwezekano kumekuwa na maeneo yenye joto zaidi nje ya mtandao wa vituo vya hali ya hewa.

-Asili ya jina "Dunia" "Earth"

Sayari zote, isipokuwa Dunia, ziliitwa majina ya miungu ya Kigiriki na Kirumi. lakini kwa upande wa sayari yetu Neno "Earth" linalotamkwa kwa kiingereza limetokana na lugha ya Kijerumani ya zamani "ertha" au "erde," ambayo inamaanisha ardhi au ardhi yenye uoto wa mimea. kuna majina mengi ya sayari yetu katika maelfu ya lugha zinazozungumzwa na watu wa sayari hii ya tatu kutoka lilipo Jua.

Neno "Dunia" tunalolitamka kiswahili limetokana na Lugha ya Kiarabu "Addunya".

Kwa kumalizia, kujifunza zaidi kuhusu dunia yetu kunaweza kuwa ni safari ya kushangaza. Tunapogundua zaidi kuhusu mazingira yetu, tuchukue jukumu la kuitunza na kuithamini. Elimu ni ufunguo wa kuelewa upekee wa dunia yetu na jinsi tunavyoweza kuchangia katika kutunza hazina hii adimu. 

Ndio! Tunaishi duniani, na dunia yetu ipo ndani ya ulimwengu uliojawa nyota na mwezi ikidaiwa kuwepo sayari nyingine nyingi. Hivi ni kweli tuko peke yetu?

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages