Breaking

Monday 2 September 2024

DUWASA YAPONGEZWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI KONGWA



Na. Okuly Julius Kongwa ,Dodoma


SPIKA wa Bunge Mstaafu Job Ndugai ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kuhakikisha wanashirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi ya maji.

Ndugai ameyasema hayo leo Septemba 2,2024 , wilayani Kongwa wakati akifungua kikao kazi cha DUWASA na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kujadili masuala ya huduma za maji mkoani Dodoma.

Amesema ushirikishwaji wa jamii ni muhimu ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kudumu kwa muda mrefu.

“Niwaagize DUWASA kuhakikisha mnashirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi ya maji katika hatua zote kwa sababu inatoa nafasi ya kuwajengea uelewa juu ya matumizi bora ya rasilimali za maji na hivyo kusaidia kudumisha na kulinda miradi hiyo,”amesema Ndugai

Katika hatua nyingine Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa amesisitiza kuharakisha kulipwa fidia kwa wananchi ambao wanapisha miradi ya maji.

Katika hatua nyingine Ndugai amewataka viongozi wa serikali za mitaa katika halmashuri ya wilaya ya Kongwa kuhakikisha miradi yote ya maji pamoja na vyanzo vya maji vinalindwa na kutofumbia macho aina yeyote ya uharibifu wa miundombinu ya maji inayosbabishwa na wananchi katika maeneo yao.

“kuna katabia viongozi ya kuwaficha waharibifu wa miundombinu ya maji na hii sio tabia nzuri ni vyema kila mmoja ashiriki kikamilifu kulinda vyanzo vya maji ili kuendelea kuwahakikishia wananchi huduma za maji safi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema lengo la kikao hicho ni kufahamiana na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha huduma ya maji Wilaya ya Kongwa.

Amesema hivi sasa DUWASA inaendelea na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika hasa kipindi cha kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

“Hatutaki suala la maji liwe kikwazo kwa serikali yetu katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani kwa sababu maji hayana mbadala hivyo wanachi usipowapelekea maji ya uhakika lazima tu watakuwa na maswali na ukitathmini watakuwa na haki kabisa ya kuuliza ila ukiwapelekea maji hakuna maswali,” amesema Aron

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amesema sekta ya meaji ni muhimu kwasababu inagusa wananchi moja kwa moja hivyo ameipongeza DUWASA kwa jitihada kubwa wanazoendelea nazo za kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wa Kongwa kwa uhakika.










Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages