Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, akizungumza wakati akifungua kongamano la wadau wa sekta ya Maji lililoandaliwa na Wizara ya maji kwa ajili ya kupokea maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Na Samir Salum, Langolahabari.com
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka wadau wa Sekta ya maji kutoa maoni yatakayosaidia kutatua changamoto na kuboresha sekta hiyo kwa miaka 25 ijayo.
Mhandisi Waziri ameyasema hayo leo Oktoba 10,2024 jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la wadau wa sekta ya Maji lililoandaliwa na Wizara ya maji kwa ajili ya kupokea maoni kuhusu dira ya taifa ya maendeleo 2050 kwa niaba ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso.
Mhandisi Waziri amesema sekta ya Maji bado inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira na kuwaomba wadau kutoa maoni yatayosaidia kuboresha huduma ya maji nchini.
“Sekta ya maji inakabiliwa na uchafuzi, uharibifu, uvamizi wa vyanzo vya maji na usafi wa Mazingira pia mahitaji makubwa ya fedha kwenye miradi mikubwa ya maji na mabadiliko ya tabia nchi.
“ninaomba tunapotoa maoni yetu katika mchakato wa maandalizi ya dira ya taifa ya maendeleo 2050 changamoto hizi ziangaliwe na kutokana na uzoefu na weledi nina Imani mtatoa maoni kwa mustakabali wa sekta hii miaka 25 ijayo,” amesema Mhandisi Waziri
Mhandisi Waziri ameongeza kuwa hadi kufikia Disemba 2023 Takwimu ya idadi ya watu wanaopata maji safi na salama Vijijini ni asilimia 79 huku Mijini ni asilimia 90
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya maji Prospar Mkama amesema mipango ya wizara ya maji ni kuhakikisha wanapeleka huduma ya maji maeneo muhimu ya uwekezaji ili kuendelea kuwavutia Wawekezaji.
Mkama ameongeza kuwa watahakikisha wanaendelea kujenga miundombinu rafiki ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji.
“kwa sasa tuna mpango unaoendelea wa kuchimba visima mia tisa, kwa maana kila jimbo litakuwa na visima vitano mkakati huu utatufikisha asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
“Kazi kubwa pia ni kuhakikisha tunatengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji ili wavutiwe kuwekeza nchini na kuwashirikisha wadau ili kuhakikisha tunatimiza sera ya Rais Samia ya kumtua Mwanamke ndoo kichwani, “ameeleza Mkama
Wadau walioshiriki kongamano hilo wanatoka makundi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya afya, wizara ya elimu sayansi na teknolojia, Wizara ya Kilimo na wawakilishi kutoka wizara ya nishati, Wawakilishi wa Taasisi zilizo chini ya wizara ya Maji,Mameneja wa RUWASA wa mikoa na Wilaya.
Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji, wakurugenzi wa bodi za maji za mabonde, Chuo cha Maji, Mfuko wa Taifa wa Maji, wawakilishi wa taasisi za umma ikiwemo tume ya taifa ya Mipango, TANAPA, TFS, EWURA, TANESCO
Wadau wa maendeleo, wadau kutoka taasisi za kidini, Asasi za Kiraia, Taasisi zisizo za kiserikali taasisi zinazojumuisha wakandarasi, washauri, na viwanda vya uzalishaji wa maji.