*Dk. Mwasaga apongeza mchango wa sekta binafsi
Na Mwandishi Wetu*
TUME ya TEHAMA nchini (ICTC) imesaini makubaliano ya kuanzishwa rasmi kwa ushirikiano na kampuni ya Soft-Tech Consultant Ltd kwa lengo la kuimarisha sekta ya TEHAMA na kutoa fursa zaidi kwa vijana wa Kitanzania kupata ajira kupitia ubunifu wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa Mkataba wa ushirikiano huo katika Ofisi za Tume zilizipo Upanga, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema kuwa sekta binafsi imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza TEHAMA, hivyo ushirikiano huo unaimarisha juhudi za pamoja za kukuza teknolojia kwa manufaa ya taifa.
“Tanzania ina vijana wengi wenye uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya uchumi. Ushirikiano huu utaleta fursa mpya za ajira, ubunifu, na ushindani wa vijana wetu katika soko la Afrika na dunia,” alisema Dkt. Mwasaga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Soft-Tech Consultant Ltd, Harish Bhatt, alisema kampuni hiyo yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 33 na iliyofanya kazi katika nchi mbalimbali barani Afrika, inaamini katika nguvu ya ushirikiano na taasisi za umma kama njia ya kuleta mageuzi ya kidijitali.
“Tunatambua mchango mkubwa wa Tume ya TEHAMA katika kujenga mazingira rafiki ya teknolojia, na tuko tayari kushirikiana nao kuanzisha mifumo itakayokuwa na athari chanya sio tu nchini, bali kimataifa,” alisema Bhatt.
Ushirikiano huo unalenga kufanya tafiti za kisayansi, kuanzisha mifumo ya TEHAMA, na kutoa mafunzo kwa vijana ili kuongeza ujuzi na uwezo wao katika teknolojia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutekeleza maono ya Serikali ya Tanzania chini ya Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan ya kukuza uchumi wa kidijitali.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga akiwa na Mkurugenzi Kampuni ya Soft-Tech Consultant Ltd, Harish Bhatt, baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano katika kukuza kuimarisha sekta ya TEHAMA na kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kupata ajira kupitia ubunifu wa Kidijitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga (katikati) na Mkurugenzi Kampuni ya Soft-Tech Consultant Ltd, Harish Bhatt (kushoto kwa Dkt. Mwasaga wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Tume na wale sa Soft-Tech baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano katika kukuza kuimarisha sekta ya TEHAMA na kutoa fursa kwa vijana wa Kitanzania kupata ajira kupitia ubunifu wa Kidijitali.