Breaking

Tuesday, 27 May 2025

MWANZA YASIMAMA: USIKU WA TUZO ZA MDAU SHUPAVU WAZUA HAMASA MPYA YA MAENDELEO NA UZALENDO

 

 Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Taasisi ya HolySmile imeandika historia mpya katika sekta ya maendeleo ya kijamii kwa kuandaa kwa mafanikio makubwa Usiku wa Wadau Shupavu na Tuzo za Mdau Shupavu – Msimu wa Kwanza, tukio ambalo limefanyika usiku wa Mei 25, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwanza Hotel  Jijini Mwanza.

Tukio hilo, ambalo lilikusudia kutambua, kuthamini na kuhamasisha mchango wa watu binafsi, taasisi na makundi mbalimbali katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni, limehudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi, wadau wa maendeleo kutoka sekta mbalimbali, waandishi wa habari pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Said Mtanda, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Thomas Swalala ,ameipongeza Taasisi ya HolySmile kwa kuandaa tukio hilo muhimu huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano, ushiriki wa wananchi katika maendeleo, pamoja na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kama sehemu ya kuendeleza uzalendo na demokrasia nchini.

“Mshikamano wetu, ushiriki wa kijamii, na demokrasia ni nguzo muhimu za maendeleo ya kweli. Uchaguzi ni fursa ya kila Mtanzania kuamua mustakabali wa taifa letu”, amesema mgeni rasmi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya HolySmile, Ndugu Arnold Bweichum, amewashukuru wadau wote waliojitokeza na kuhimiza kuendelezwa kwa ushirikiano wa pamoja katika kuleta maendeleo endelevu.

“Tunajivunia kuwa jukwaa la kuenzi na kuhamasisha kazi nzuri zinazofanywa na watu wa kawaida katika jamii. Tunataka kuendelea kuibua vipaji na nguvu mpya zitakazochochea mageuzi chanya si Mwanza tu bali Tanzania nzima,” amesema Bweichum.

Tukio hilo limejumuisha utoaji wa tuzo mbalimbali zenye lengo la kutambua na kuenzi juhudi za watu binafsi na makundi waliotoa mchango mkubwa katika sekta kama afya, elimu, kilimo, biashara, sanaa, utamaduni, mazingira, ujasiriamali, na usalama wa jamii.

Zaidi ya hayo, Tuzo 13 za kushindaniwa kwa kura za wazi, Tuzo 3 za heshima kwa viongozi wakuu wa Mkoa na Wilaya pamoja na Tuzo 20 za Wadau Shupavu waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, zimetolewa katika usiku huo wa kipekee.

Mbunge wa Vijana CCM Taifa kutoka Mkoa wa Mwanza, Mhe.  Ng’wasi Kamani amepokea Tuzo ya Heshima na kutoa shukurani kwa wadau wote kwa usaidizi wao katika kufanikisha maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla.

“Tuzo hii ni faraja kubwa na itanisukuma zaidi kuendelea kutumikia kwa moyo wote. Nitashirikiana na wadau wote kuhakikisha maendeleo haya yanaendelea kuimarika,” amesema Mbunge Kamani.

Kwa ujumla, Usiku wa Wadau Shupavu na Tuzo za Mdau Shupavu umeonyesha kuwa kwa mshikamano na ushiriki wa kila mtu, jamii yetu inaweza kufanikisha maendeleo endelevu na kuwa na nguvu za kuleta mabadiliko chanya.
Mkurugenzi wa Taasisi ya HolySmile, Ndugu Arnold Bweichum akizungumza katika Usiku wa Wadau Shupavu na Tuzo za Mdau Shupavu – Msimu wa Kwanza Mkoa wa Mwanza


 

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages