
Na Samir Salum
Wizara ya Katiba na Sheria imefanikiwa kutoa elimu Na huduma za kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia kupitia mikutano na huduma za ana kwa ana.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Alisema kuwa wizara imefanikiwa kutoa elimu na huduma za kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia kupitia mikutano na huduma za ana kwa ana.
“Jumla ya wananchi 2,698,908 wamepata huduma hizi na jumla ya Halmashauri 180, kata 1,907, vijiji na mitaa 5,702 na mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani”
“Wananchi hao wamepata huduma isipokuwa mkoa wa Dar es Salaam. Wamefikiwa na Kampeni hii na mkoa wa Dar es Salaam utafikiwa Mapema Juni 2025.” alisema Dkt. Ndumbaro
Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa wizara imefanikiwa kutoa elimu ya Uraia na haki za binaadam pamoja na elimu ya Utawala Bora kwa wananchi zaidi ya milioni sita katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu tassan.
Alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 Wizara imetoa elimu ya haki za binaadam, Uraia na utawala Bora ili kuhakikisha ila mtanzania anatambua yeye ni nani na wajibu wake ni nini.
“Wizara yetu ni Wizara ya haki, imepewa mamlaka ya kusimamia Katiba, Sheria na haki ndio maana katika kipindi hiki cha Uongozi wa Awamu ya sita tumefarikiwa kutoa elimu kwa wananchi milioni Sita kwa mikoa yote, wiki Iliyopita tumetoa elimu kwa zaidi ya wananchi 10,000. Mkoani Ruvuma na wiki ijayo timu ya wataalam inajipanga kuelekea mkoani Mbeya” alisema Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa idadi ya Mashirika yanayotoa Huduma za Msaada wa Kisheria yameongezeka kutoka 84 Novemba, 2021 hadi 377 mwaka 2025 huku idadi ya Wasaidizi wa Msaada wa Kisheria imeongezeka kutoka 617 mwaka 2021 hadi 2,205 mwaka 2025.
Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025 wizara ya katiba na Sheria imefanikiwa kutunga na kufanya marekebisho ya Sheria kuu 57 kati ya 446 na Sheria ndogo zaidi ya 4,000 kati ya Sheria 4887, huku Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Tanzania ilisajili jumla ya wanafunzi 5,333 sawa na asilimia 28 ya wanafunzi 19,025 waliosajiliwa katika miaka 18 tangu Kuanzishwa kwa Taasisi.
Aidha, katika kipindi hicho, Taasisi iilito wahitimu 2,375 sawa na asilimia 25 ya wahitimu 9,629 waliohitimu tangu kuanzishwa Kwa Taasisi mwaka 2008 na kufanya jumla ya Mawakili 2,375 wameongezeka katika Sekta.