Breaking

Thursday, 24 February 2022

OFISI YA WAZIRI MKUU YATOA TAHADHARI KUFUATIA MVUA ZA MASIKA


SERIKALI imetoa tahadhari kwa wananchi kufuatia mvua za masika za Machi hadi Mei, 2022 zinazoendelea kunyesha katika mikoa inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Dkt. Pindi Chana (Mb) ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2022 jijini Dar es Salaam na kusema kuwa mikoa ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki katika Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Ukanda wa Pwani ya Kaskazini katika Mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Tanga, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, visiwa vya Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Ukanda wa ziwa Victoria Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Amesema kuwa tahadhari hiyo inakuja kufuatia taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inayoonesha kuwa mvua hizi zitakuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.

Amesema Madhara yanayoweza kujitokeza katika sekta mbalimbali ikiwemo matukio ya magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea yanaweza kujitokeza kutokana na hali ya unyevuunyevu, kutuama kwa maji na kuchafuka kwa maji.
  
Amesema ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi na kuathiri shughuli mbalimbali hususani katika maeneo ya wachimbaji madini wadogo.


Dkt. Pindi Chana ameomba Serikali na wadau kuchukua hatua stahiki kuhakikisha matumizi bora ya mvua hizo pamoja na hatua za kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea.


"Tuhakikishe mvua hizi zinatumika kwa shughuli za maendeleo ikiwemo; kilimo, kuandaa mabwawa na malango kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa samaki, kuandaa malisho na nyasi za akiba za mifugo.Kuandaa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu na wanyama kama homa ya matumbo na kipindupindu na magojwa ya milipiko ya mifugo." Amesema Dkt. Pindi Chana.

Aidha Serikali imetoa pole kwa wale wote ambao walipitia kipindi kigumu kutokana upungufu wa mvua za Vuli (Oktoba, Novemba na Disemba 2021) kwa Mikoa inayopata misimu miwili kutokana na uhaba wa malisho na maji kwa mifugo kwasababu hali hiyo ilisababisha baadhi mifugo kudhoofika na kufa kutokana na njaa na magonjwa nyemelezi.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages