
Alex Sonna _CHAMWINO
WANACHAMA wa JUKWAA la Ushirika Mkoa wa Dodoma wametimiza kwa vitendo msingi wa Saba wa Ushirika wa kuijali jamii kwa kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 14 kwa Hospitali ya wilaya ya Chamwino iliyopo katika kijiji cha Mlowa barabarani kilichopo wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Wiki ya Jukwaa la Ushirika imeanza Jana Mei 10 kwa kufanyika Bonanza katika uwanja wa Kilimani Jijini hapa na itaendelea kwa wiki nzima ambapo kitakuwa na semina na wanajukwaa watapata nafasi ya kutembelea mbuga za Wanyama na vivutio mbalimbali vya Utalii.
Akizungumza leo Mei 11,2025 katika Hospitali hiyo,Mrajis Msaidizi Mkoa wa Dodoma Bw.Joseph Chitinka amesema wameungana na wanaushirika kwa ajili ya kutoa msaada wa vifaa tiba lengo likiwa ni kutekeleza kwa vitendo msingi namba saba wa kuijali jamii.
Amesema vifaa hivyo vinathamani ya zaidi ya Sh milioni 14 zilizochangwa na wanaushirika ili kukidhi yale mahitaji ya msingi ambayo jamii imekuwa ikikutana nayo.
"Sisi tunahudumia jamii na tuna maadhimisho yetu kwahiyo hizi ni shamrashamra tunaamini huu misaada itawasaidia,"amesema Chitinka.
Hata hivyo ametoa wito kwa taasisi zingine kuendelea kutenga mafungu kwa ajili ya kuwasaidia wale wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Jukwaa la Ushirika Mkoa wa Dodoma, Ibrahim Sumbe amesema wanamshukuru Mungu kwa kuweza kuwafikisha Mlowa Wilaya ya Chamwino kwa ajili ya kutoa msaada ili kuwasaidia wenye mahitaji na wagonjwa.
"Leo ni mwendelezo wa kuigusa jamii kwa vitendo kwahiyo tuna vifaa,tiba,vitanda,Viti mwendo na vifaa vingine kwa ajili ya watoto na kina mama katika Hospitali hii ya Chamwino,"amesema Sumbe.
Hata hivyo,Mwenyekiti hiyo ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma ambao ni wanaushirika kujiunga na jukwaa hilo kwa ngazi zote kwa sababu unagusa katika maeneo yote.
Naye,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chamwino Dk Idan Nchimbi amewashukuru wanaushirika kwa kufika na kuwapatia vifaa hivyo ambavyo Moja kwa Moja vitagusa maisha ya watanzania.
Amesema Nchi ni kubwa kuna Halmahsuari zaidi ya 184 ambapo Serikali inajitahidi kujenga vituo vya afya lakini Kuna baadhi ya mahitaji ni lazi a yatolewe na wadau kama wanaushirika.
"Tunapopata ugeni kama huu kwa kweli inaleta furaha hichi kitu kinaenda moja kwa moja kwenye jamii,nitoe wito kwa taasisi vingine kuendelea kuiunga mkono Serikali hasa katika sekta ya afya kwa sababu mahitaji ni makubwa lakini Serikali yetu imekuwa ikihakikisha kila kitu kinapatikana Tena kwa wakati,"amesema Dk Nchimbi



















