Tuzo hizo zilizotolewa katika hafla iliyofanyika Mei 5, 2025, katika ukumbi wa Super Dome Jijini Dar es salaam zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanahabari, na wadau wa maendeleo, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.
Katika hafla hiyo iliyopambwa kwa shamrashamra na heshima ya juu, Dotto Dosca Kwilasa ametambuliwa kwa kazi yake bora na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemkabidhi Dotto Dosca Kwilasa, zawadi ya shilingi Milioni tano, cheti, madini ya Rubi pamoja na Leseni ya Utafiti wa Madini yenye ukubwa wa kilomita za mraba 20.
Dotto Kwilasa ambaye ni mwandishi wa habari, mtengenezaji na mchapishaji maarufu wa maudhui Mtandaoni ametambulika kwa uchambuzi wake makini, weledi wa hali ya juu, na matumizi bora ya teknolojia ya habari kuibua na kufikisha habari zenye tija kwa jamii.
Malunde Media inayomiliki mtandao wa Malunde 1 blog, chini ya uongozi wa Kadama Malunde ambaye ni mwandishi wa habari mahiri akitokea mkoani Shinyanga, inaendelea kung’ara katika uandishi wa habari za maendeleo, huku ikitoa nafasi kwa waandishi wachanga na mahiri kama Dotto Kwilasa kung’ara katika ulingo wa habari kitaifa na kimataifa!
Tuzo za Samia Kalamu Awards zimeanzishwa kwa lengo la kutambua mchango wa waandishi wa habari nchini Tanzania katika kuhamasisha maendeleo kupitia kalamu zao, zikilenga sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, madini, mazingira, na utawala bora.
Dotto Dosca Kwilasa sasa anabaki kuwa kielelezo cha uandishi wa kisasa unaogusa jamii, unaoibua fursa na kuhamasisha maendeleo ya kweli kupitia kalamu yenye uzito na dhamira ya dhati.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Viongozi, Wadau wa habari pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya utoaji wa Tuzo za Samia Kalamu Awards 2025 kwa Waandishi wa Habari katika ukumbi wa The Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 05 Mei, 2025.




