
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Omary Mugisha (42) mfanyabiashara katika Soko la Mwenge Jijini Dar es Salaam amefariki akiwa amenasa juu ya paa la nyumba lililokuwa na umeme.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhani Kingai kusema kuwa tukio hilo limetokea leo Jumatano Aprili 13, 2022 majira ya asubuhi.
ACP Kingai, amesema kwamba Omary alikuwa akijaribu kujiunganishia umeme na kwamba pembeni yake kulikuwa na kifaa cha kukatia nyaya pamoja na waya wa umeme huku akiwa ameshikilia bisibisi.
"Ni kweli huyo Bwana alikutwa kwenye paa la nyumba akiwa amefariki kwa kupigwa na shoti ya umeme, ni kwamba alikuwa akijiunganishia umeme katika kibanda chake. Hakua na vifaa kinga kama gloves, lakini tumemkuta akiwa na waya pamoja na pisipisi mkononi. Mwili wake umehifadhiwa hospitali ya Mwananyamala kwa utambuzi" - Amesema
Kwa upande wake M/kiti wa mtaa wa Mwenge, Bashir Hozza amesema kuwa marehemu alikuwa akijaribu kujiunganishia umeme kiholela usiku katika kibanda chake.
"Huyu Bwana alikuwa anajiunganishia umeme na hii ni kazi ambayo amekuwa akiifanya kinyume cha sheria. Kwahiyo kama mlivyoona huyu ni mzembe. Alipanda bila hata tahadhari, hana gloves, hana viatu na mvua ilivyokuwa imenyesha akanaswa na umeme" - amesema Mwenyekiti