Breaking

Saturday 21 May 2022

HALIMA KOPWE ASHINDA TAJI LA MISS TANZANIA 2022, RAIS SAMIA KUJENGA UKUMBI WA KIMATAIFA DAR




Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Mhe. Rais Samia imedhamiria kuinua kuinua kiwango cha mashindano ya urembo nchini ikiwa ni pamoja na kujenga ukumbi wa kimataifa katika jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo Mei 21, 2022 kwenye kilele cha mashindano ya kumtafuta Miss Tanzania 2022 ambapo Halima Kopwe toka Mtwara ametwaa taji hilo, Waziri Mchengerwa amesema ukumbi huo licha ya kufanyiwa kazi mbalimbali za Sanaa na burudani pia utatumika kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na shindano la Miss Tanzania.

"Ukumbi huo unatarajiwa kuongoza kwa ubora na ukubwa barani Afrika ambapo utachukua takribani watu elfu ishirini" amesisitiza Mhe. Mchengerwa


Amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwashika mkono washindi wote na kufafanua kuwa washiriki wote walioshiriki shindano hili hadi kufika fainali ni washindi.

Amewapongeza waandaji wa shindano hilo kwa uratibu mzuri ambapo ameongeza kuwa washiriki wamefanya kazi nzuri ya ubunifu na Sanaa


Aidha Waziri Mchengerwa amesema Filamu ya Royal Tour imesaidia kufungua milango na kuitangaza Tanzania duniani na kuwataka wasanii kutumia fursa hiyo kutengeneza ajira na vipato.


Miss Tanzania kwa mwaka huu; Halima Kopwe amejishindia gari dogo aina ya Benzi lenye thamani ya shilingi milioni 30 na fedha taslimu shilingi milioni kumi.



Shindano hilo limefanyika jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na mamia ya washabiki wa urembo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages