Breaking

Saturday 21 May 2022

TPAWU YAMUANGUKIA RAIS SAMIA NYONGEZA YA MISHAHARA




Na Mwandishi Wetu, Morogoro

IKIWA imepita wiki moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuongeza mshahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3 Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani Tanzania (TPAWU), kimemuomba Rais kufanya hivyo na sekta binafsi ambayo ina miaka tisa bila kuongezwa mshahara.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa TPAWU Taifa Fred Akondowe wakati akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Morogoro kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi ambapo walikutana kujadili suala hilo, kupitisha bajeti ya chama na kuzindua tovuti yao.

Akondowe alisema wafanyakazi wa sekta binafsi hasa wa mashambani wamekuwa wakipitia wakati mgumu kwenye maisha kutokana na mshahara mdogo ambao wanapatiwa na waajiri wao.

“Sisi tuna miaka tisa mshahara haujaongezeka na kima cha chini kwa wafanyakazi wa mashambani ni shilingi 100,000, hivyo tunaomba Rais Samia aone kundi hili nalo kama ambavyo ameona kwa watumishi wa umma,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wanaomba kima cha chini kwa wafanyakazi wa mashambani kiwe Sh.700,000 ili waweze kukidhi mahitaji yao, kutokana na ukweli kuwa bei za bidhaa zimepanda kwa kasi kubwa.

Alisema alichofanya Rais Samia ni ushahidi tosha kuwa anajali wafanyakazi, hivyo imani hiyo aihamishe kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ambao ndio wenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo.

Akondowe alisema wafanyakazi wa mashambani wanafika 50,000 hivyo ni vema Serikali inapaswa kuangalia kundi hili ambalo linachangia utajiri wa watu binafsi na Serikali.

Alisema kitendo cha kutopanda mshahara kwa miaka tisa kimesababisha chama kufanya kazi katika mazingira magumu, hivyo ni imani yao neema ya nyongeza itawafikia.

“Sisi hatutaki milioni 1 tufike hata laki saba, kwani hili kundi ndilo linazalisha chakula cha Watanzania wote ni lazima lipewe kipaumbele,” alisema

Katibu Mkuu wa TPAWU Kabengwe Ndebile alisema wajumbe wa kikao hicho kwa pamoja wamekubaliana kusimama na wadau wote wa sekta binafsi kuhakikisha mshahara unaongezwa kulingana na hitaji husika.

“Sisi tumetuma wawakilishi wetu kwenye kikosi ambacho kinachakata mshahara sekta binafsi ili na sisi tupate neema, kwa sasa kinachotulinda ni kutokana na aina ya mikataba ambayo imekuwa ikiongeza mshahara kidogo kidogo,” alisema

Katusime Kafanabo Katibu wa Idara ya Elimu, Wanawake na Vijana TPAWU, alisema kutokuongezwa mshahara kwa fanyakazi wa sekta binafsi ni kudidimiza uchumi na maendeleo.

Alisema iwapo hakutakuwa na uongezeko la mshahara ni dhahiri kuwa kundi hilo litaendelea kuwa maskini mwaka hadi mwaka.

“Mshahara wa kundi hili upo chini sana, kwani sh.100,000 haiwezi kulipia ada, afya, na huduma nyingine muhimu kwa mwanadamu. Sisi tuna fursa za kufunga mkataba wa kima cha chini ila hali ilivyo sasa ni dhahiri hata hicho kinachofungwa hakina tija,” alisema.

Kafanabo alisema TPAWU inahamasisha vijana na wanawake kujiunga na chama, ili waweze kushirikiana kuchochea maendeleo na uchumi wa nchi.

Katibu huyo alimuomba Rais Samia kutumia nafasi yake kuwaonea huruma wafanyakazi wa sekta binafsi hasa wanawake wenzake ili waweze kupata mishahara sahihi itakayochochea maendeleo.

Aidha, Kafanabo alisema TPAWU katika kukimbizana na maendeleo ya teknolojia wamezindua tovuti ambayo itaweza kuwasaidia kutoa mafunzo na kuwasiliana na wanachama wao kirahisi.

Naye Katibu wa TPAWU Kanda ya Mashariki, Nichaus Ngowi alisema Serikali inapaswa kutambua mchango wa sekta binafsi ambayo ni injini ya uchumi wa nchi.

Ngowi alisema Tanzania haiwezi kupata maendeleo iwapo sekta binafsi itaachwa nyuma katika eneo la maslahi.

Mei 14 mwaka huu Rais Samia aliridhia mapendekezo ya kuongeza mishahara ikiwemo kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambapo Sh1.59 trilioni itatumika kwa ongezeko hilo.



Hatua hiyo ya Rais Samia ilikuja ikiwa ni baada ya mapendekezo ya mwendelezo wa kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alichokifanya mkoani Dodoma na kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu kuhusu ongezeko la mishahara.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ilisema Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh.trilioni 9.7 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishara ya watumishi wote katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala za Serikali.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages