Breaking

Monday 16 May 2022

KATIBU MTENDAJI TUME YA MADINI AWATAKA WACHIMBAJI KUSHIRIKI SENSA



Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kuweka mikakati ya namna bora ya kutoa huduma kulingana na idadi yao.


Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Mei 16, 2022 kwenye ufunguzi wa mafunzo  kuhusu usimamizi wa usalama, afya, mazingira, usimamizi wa baruti pamoja na sheria za madini kwa wadau wa madini ya vito mkoani Manyara yaliyofanyika katika mji wa Mirerani ambayo yamekutanisha wamiliki wa  migodi, wachimbaji wadogo wa madini na walipuaji wa baruti.



Amesema kuwa lengo la sensa katika ngazi ya kitaifa ni kuiwezesha serikali kuweka mikakati ya kuboresha huduma za jamii kama vile miundombinu, afya, elimu na kuongeza kuwa katika ngazi ya Sekta ya Madini ni pamoja na kuiwezesha Serikali kufahamu idadi halisi ya wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini na namna bora ya kuwasaidia kwa kusogeza huduma  karibu na maeneo yao.


“Sensa hii itaisaidia Serikali kupitia Wizara ya Madini kubaini maeneo yenye  wachimbaji wengi wa madini na mahitaji na kusogeza huduma kama vile ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa na masoko ya madini,” alisema Samamba.


Amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanaimarisha mahusiano na  jamii inayozunguka migodi yao kwa kuboresha huduma za jamii kama vile maji, elimu, afya, miundombinu kama sheria ya madini inavyotaka.



Aidha, Mhandisi Samamba amewataka wananchi kuhakikisha wanachangamkia fursa za uwekezaji zilizopo kwenye shughuli za uchimbaji na biashara  ya madini kwa utoaji wa huduma kama vile ulinzi, vyakula, usafiri na kujipatia kipato baada ya kuwepo kwa ongezeko la wafanyabiashara kwenye biashara ya madini katika eneo la Mirerani.


“Serikali imefungua fursa kwa kuhakikisha shughuli za uchimbaji na biashara ya madini zinafanyika katika eneo la Mirerani kama hatua mojawapo ya kuinua uchumi wa Mirerani sambamba na kuinua uchumi wa nchi.


Aidha, amewataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanaajiri wataalam wa madini na ulipuaji wa baruti ili kuzuia ajali zinazoweza kujitokeza mara kwa mara kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.


Amesisitiza kuwa serikali ina mkakati wa kuhakikisha wachimbaji wadogo wanachimba madini na kupata faida na serikali kukusanya mapato yake bila kuathiri afya na mazingira ya jamii inayozunguka.

Naye Mkuu wa Wlaya ya Simanjiro, Dkt. Suleiman Serera akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo amesema kuwa Serikali imejipanga kuboresha mazingira ya kazi ya wachimbaji wadogo wa madini katika eneo la Mirerani kwa kuimarisha usalama na kuanza ujenzi wa soko la madini.

 

Serera ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa wananchi wengi wameanza kunufaika.

 

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages