Breaking

Friday 20 May 2022

MACHINGA KUTUNGIWA SHERIA YA KUWALINDA



Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema Serikali imeanza mchakato wa kutunga Sheria ya kuwalinda wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama 'machinga'.


Dkt. Zainab ametoa kauli hiyo  jijini Dodoma Mei 19, 2022 wakati akifunga mafunzo kwa viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA).


Katika hatua nyingine Dkt. Chaula ametumia nafasi hiyo kutoa mwezi mmoja kwa mikoa ambayo haijakamilisha usajili wa wanachama wa Shirikisho hilo kufanya hivyo ili kuwepo takwimu sahihi za wanachama zitakazosaidia kuhudumia kundi hilo.


Dkt. Chaula ameongeza kuwa shabaha ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kundi la machinga linaratibiwa vizuri na linapata fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo mikopo na masoko ya bidhaa zao.


"Ndio maana Rais Samia akaunda Wizara hii na kuipa jukumu la kuratibu makundi Maalum ikiwepo kundi la Machinga kwa sababu Serikali inawajali na kuwathamini Machinga kama yalivyo Makundi mengine waliopo ndani ya jamii' alisema Dkt. Chaula


Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Shirika la Posta, NSSF, ASAS na wadau wengine waliandaa mafunzo kwa viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi na kuweka mikakati ya uendeshwaji Shirikisho lao. 

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages