Breaking

Thursday 5 May 2022

MAWAZIRI WAKUTANA KUTAFUTA MBADALA WA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.


Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi yaWaziri Mkuu leo Alhamisi, Mei 5, 2022 imeeleza kuwa kikao hicho kimefanyika usiku wa kuamkia leo kwenye ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.

"Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi," amesema.

Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.

"Mheshimiwa Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii," amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.

"Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza, kwa kutathmini maombi 24 ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata. Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” amesema.




Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya mawaziri akiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, January Makamba, Makatibu Wakuu, pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), kimefanyika siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages