Breaking

Sunday 15 May 2022

WATOA HUDUMA KWENYE SHEREHE WATAKIWA KUWA WABUNIFU




Na John Mapelele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema huu ni wakati wa kuongeza ubunifu kwenye utendaji kwa tasnia ya utoaji wa huduma katika sherehe ili kutoa ajira na kuongeza vipato vyao kwa ujumla.

Waziri Mchengerwa ametoa wito huo leo Jumapili Mei 15, 2022 katika wakati akitoa hotuba yake kwenye kilele cha maonesho ya tano ya biashara yanayowajumuisha watoa huduma wote kwenye sherehe baada ya kukagua mabanda yote ya washiriki Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Watoa huduma hao ni pamoja na washereheshaji, wauzaji wa nguo za harusi, wapishi, wapiga picha wenye saloon na watengenezaji keki.


Mchengerwa amewataka wanatasnia kuendeleza umoja baina yao kwa madai kuwa sekta hizo za Utamaduni, Sanaa na Michezo ni nguvu shawishi ya Serikali inayosaidia kuleta amani, mshikamano na furaha kwa wananchi huku akiwataka kutumia mashirikisho yao ili iwe rahisi kwa Serikali kutatua changamoto zinaziwakabili.

Amesema Serikali itaendelea kuwajali kwa kuwa shughuli za sherehe zinatoa ajira kwa watu wengi hapa nchini.


Kuhusu Serikali kutoa mikopo kwa watoa huduma amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa 1.5 bilioni kwa ajili yao na kuwaomba kuwasilisha maandiko Serikalini kupitia mashirikisho yao ili waweze kupata mikopo hiyo bila riba yoyote.

Aidha, kuhusu kuwa na kumbi kwa ajili ya watoa huduma amefafanua kuwa Serikali inadhamiria kujenga ukumbi wa Sanaa na Maonesho jijini Dar es Salaam ambao utachukua takribani watu 20000 kwa mara moja.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Adorable Wedding Trade Anna Lema amemshukuru na kumpongeza Waziri Mchengerwa kwa kusimamia vizuri sekta anazoziongoza.

Katika tukio hilo Mhe, Mchengerwa ametoa vyeti kwa washiriki wote wa onesho hilo na kukata keki ya miaka mitano ya taasisi ya maonesho ya "Adorable Wedding Trade" kwa kutimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.


Pia Mhe. Mchengerwa amechezesha droo kwa ajili ya kuwapata wachumba wanaotarajia kufunga ndoa watakaogharimiwa kwa asilimia 80 na taasisi hiyo ambapo Isaac Miraji Msofe na Diana Tangira wameibuka washindi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages