Breaking

Thursday 5 May 2022

WAZIRI DKT. GWAJIMA ATOA MREJESHO MIKUTANO YA KIMATAIFA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, akifungua kikao cha tathmini ya Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani na Mkutano wa G7, Mikutano ambayo Mhe. Waziri alihudhuria akiwa na wataalam wa Tanzania kwa Nyakati Tofauti nchini Marekani na Ujerumani.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula akitoa maelezo ya awali katika kikao cha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipotoa tathmini ya Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani na Mkutano wa G7 katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akizungumza katika kikao cha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, alipotoa tathmini ya Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani na Mkutano wa G7 katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Wawakilishi kutoka Wizara, Taasisi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine wakiwa katika kikao cha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipotoa tathmini ya Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani na Mkutano wa G7 katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.  

***********

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima ametoa mrejesho wa mikutano miwili ya Kimataifa aliyoshiriki  ikiwemo Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani uliofanyika nchini Marekani na ule wa Mkutano wa G7 Care Work uliofanyika nchini Ujerumani.


Dkt. Gwajima akizungumza na wadau mbalimbali wa masuala ya Wanawake na Jinsia jijini Dodoma alisema Tanzania ikishiriki mikutano hiyo kwa lengo la kwenda kujifunza na kueleza Duniani nini Tanzania inafanya katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na Usawa wa Kijinsia.


"Mimi binafsi nilialikwa na nilishiriki katika mkutano huo ambapo niliambatana na mtaalamu mmoja. Mkutano huo ni muhimu sana kwa kuwa kama mnavyofahamu Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliahidi kuwa kinara wa utekelezaji wa eneo la Pili kuhusu Haki na Usawa wa Kiuchumi kwenye Jukwaa la usawa wa Jinsia" alisema Dkt. Gwajima


Aidha Dkt. Gwajima amesema lengo la Mikutano hiyo muhimu ni kujadli masuala mbalimbali ya maendeleo ya wanawake ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto zilizopo zipate maamuzi ya kisera na kiutekelezaji kutoka kwa viongozi na wataalam.


"Nimeitisha kikao hiki ili nitoe mrejesho wa mikutano hiyo miwili na pia kuweka mikakati ya utekelezaji wa maazimio ya mikutano hiyo na kupitia kikao hiki pia nitaomba tujipange vizuri zaidi ili kuwa na ushiriki bora zaidi katika mikutano hii kwa wakati mwingine" alisisitiza Dkt. Gwajima


Pia Dkt. Gwajima amewashukuru wadau waliowezesha ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani na ule wa Mkutano wa G7 Care Work ambao ni UN Women, UNFPA, Ubalozi wa Ireland na Asasi ya LSF, LANDESA na OXFAM ambazo zilichangia katika kuwezesha Viongozi na wataalam kushiriki mikutano hiyo.


"Ninaomba nitoe rai kwa wadau wengine wa Maendeleo kuendeleza ushirikiano huu na kutuwezesha kwa utaalam na rasilimali fedha na kushirikiana nasi katika maeneo mbalimbali kadri tutakavyoendelea kuwasiliana nao na kuwashirikisha kwenye maeneo yetu ya vipaumbele." alisema Dkt. Gwajima 


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula alisema Wizara imeamua kukutanisha wadau mbalimbali katika kuhakikisha inatoa mrejesho wa Mkutano wa 66 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali za Wanawake Duniani uliofanyika jijini New York Marekani na Mkutano wa G7 uliofanyika nchini Ujerumani.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa wa Dodoma upo tayari kushirikiana na Wizara na wadau wengine kuhakikisha suala la kuwawezesha Wanawake kiuchumi na Usawa wa Kijinsia ili kuwezesha kufikia azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kiuchumi na Usawa wa Kijinsia.


"Tuko tayari kabisa katika suala hili na tutahakikisha suala la uwezeshaji Wanawake kiuchumi na Usawa wa Kijinsia tulisongeshe hasa katika Mkoa wa Dodoma ili tuwe mfano" alisema Mhe. Mtaka 


MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages