Breaking

Sunday 22 May 2022

WAZIRI MCHENGERWA ATOA NENO KWA SERENGETI GIRLS KUELEKEA KOMBE LA DUNIA




Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitaka Timu ya Soka ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 ( Serengeti Girls) leo Mei 23, 2022 kucheza kufa na kupona dhidi ya Cameroon ili kujihakikishia kucheza kombe la dunia.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 22, 2022 ikiwa ni masaa machache kabla ya Serengeti Girls kushuka dimbani nchini Cameroon leo jioni kwa majira ya saa 11: 30 ya hapa nchini.

Amesema watanzania wanamatumaini makubwa na wanaiombea timu hiyo ili kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo wa soka Tanzania ishiriki katika mashindano ya dunia ambayo yanatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini India.

Ameongeza kuwa ili kufuzu kucheza kombe la dunia Serengeti Girls imebakiza kucheza na kushinda mechi mbili tu kwa maana ya mechi ya leo na ile ya marudiano itakayochezwa Juni 4, 2022 Zanzibar.

Aidha amesema mafanikio haya yanapatikana sasa kutokana na mapenzi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye michezo ambapo ametoa fedha nyingi kusaidia timu zote za taifa katika michezo mbalimbali ili ziweze kufanya vizuri na kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.

" Hapa naomba nitoe shukrani na pongezi za dhati kwa Rais wetu mpendwa, kwa mapenzi makubwa na sapoti kubwa anayotoa kwenye michezo ambayo imeleta mapinduzi makubwa" amesisitiza Mhe. Mchengerwa




Pia amefafanua kuwa kwa mara ya kwanza Timu ya Taifa ya Soka kwa Watu wenye Ulemavu ( Tembo Warriors) inakwenda kushiriki kombe la dunia Oktoba mwaka huu nchini Uturuki.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages