Breaking

Tuesday 24 May 2022

WIZARA YAWATAKA WAFANYABIASHARA WA MADINI KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza wakati wa ziara yake na naibu waziri wa Zimbabwe ya kutembelea wachimbaji wadogo katika mgodi wa Kadeo Leo Mei 24, 2022
Naibu waziri wa madini Zimbabwe Dkt. Mhandisi Polite Kambamura akizungumza alipotembelea maeneo ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa Kadeo
Balozi wa Zimbabwe Nchini Lt. Gen. Anselem Sanyatwe akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo ya wachimbaji wadogo katika mgodi wa Kadeo
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa na Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe na ujumbe wake wakiwa katika mgodi wa Kadeo ili kujifunza masuala mbalimbali kuhusu wachimbaji wadogo wanavyofanya kazi
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa (kulia) akimuonyesha bei elekezi ya madini naibu waziri wa madini Zimbabwe (Katikati) walipotebelea soko la madini Lwamgasa mkoani Geita leo Mei 24, 2022
Wachimbaji wadogo wa madini katika mgodi wa Kadeo Mkoani Geita

********

WAFANYABIASHARA wa madini nchini wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa kwenye Sekta ya Madini kuanzia katika uzalishaji, uchakataji, uongezaji thamani na utafutaji wa masoko.


Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ametoa wito huo leo Mei 24, 2022 wakati wa ziara ya naibu waziri wa madini wa Zimbabwe, Dkt. Mhandisi Polite Kambamura alipotembelea soko kuu la dhahabu mkoani Geita.


Dkt.Kiruswa amesisitiza wafanyabiashara wa madini na wachimbaji kuhakikisha wanaheshimu sheria zilizopo nchini ikiwemo kulipa kodi stahiki kwa taratibu zilizowekwa.


Kuhusu bei elekezi inayotolewa kwenye masoko ya madini amesema, bei hiyo imepangwa kulingana na viwango vilivyopo kwenye soko la Dunia hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kuzingatia bei elekezi na kuacha kujipangia bei yao wenyewe.


"Nitoe wito kwa wafanyabiashara wa madini ambao wanajaribu kwenda kuwaomba wale wanaowauzia washushe chini ya bei elekezi ya Serikali, jambo hilo haliruhusiwi," amesisitiza Dkt.Kiruswa.


Kwa upande mwingine, Dkt.Kiruswa amewapongeza wafanyabiashara wa madini katika soko la dhahabu Geita ambao wamemhakikishia kuwa wanazingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zinazosimamia Sekta ya Madini ikiwemo kuzingatia bei elekezi iliyopangwa.


Pia, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji nchini.


Aidha, amempongeza Naibu Waziri wa Zimbabwe na ujumbe wake ambao wamefika nchini kujifunza shughuli zinazohusu Sekta ya Madini ikiwemo uchimbaji.


Naye, Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe, Dkt.Mhandisi Polite Kambamura amesema, Sekta ya Madini nchini Tanzania imekuwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo ya wachimbaji wadogo jambo lililowapa hamasa na wao kufika nchini kujifunza.


Naye, Balozi wa Zimbabwe nchini, Luteni Jenerali Anselem Sanyatwe ameishukuru wizara kwa kutoa fursa kwa Wizara ya Madini ya Zimbabwe kufika Tanzania kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini.


Pia, ameridhishwa na uendeshaji wa masoko ya madini nchini jambo lililopelekea kupata masoko ya uhakika kwa wafanyabiashara.


Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe na ujumbe wake wameshiriki ziara ya siku mbili mkoani Geita na Mwanza yenye lengo la kujifunza kuhusu shughuli za uchimbaji madini nchini.


Aidha, wametembelea maeneo ya wachimbaji wadogo waliopo Lwamgasa mkoani Geita kujifunza shughuli za uchimbaji, uchakataji na uchenjuaji wa madini

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages