Breaking

Wednesday 8 June 2022

JAJI MSTAAFU KALOMBOLA ATOA WITO KWA WATUMISHI WA TUME KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mheshimiwa Hamisa H. Kalombola ametoa wito kwa Watumishi wa Tume kufanya kazi kwa kushirikiana, bidii, weledi na uzalendo ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa.

Mheshimiwa Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola amesema hayo jana alipokutana na Watumishi wa Tume wakati wa ziara yake katika Ofisi za Tume ya Utumishi wa Umma, Jijini Dodoma aliyoifanya kwa lengo la kukutana na Watumishi wa Tume na kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.

“Tume hii ina taswira nzuri na watu wana imani na sisi katika kazi tunazozifanya. Sijasikia habari zenye kuipa Tume yetu taswira mbaya najua mnafanya vizuri, sasa shime shikamaneni, mshirikiane na mhakikishe mnailinda taswira nzuri iliyopo. Epukeni kufanya vitendo visivyofaa na habari mbaya zenye kuichafua Tume ya Utumishi wa umma” alisema Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kwa watumishi wa Tume, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola alisema kuwa watumishi wanapaswa wakati wote kufahamu kuwa jambo kubwa katika utendaji wa kazi ni kushirikiana, kuzingatia maadili, kufanya kazi kwa pamoja, kwa kutambua kuwa watumishi wakipambana katika kazi wakiwa wengi na kwa pamoja kazi inakuwa rahisi na pale kwenye changamoto inakuwa ni rahisi kuzitafutia ufumbuzi na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea.

“Tufanye kazi kwa pamoja, sifa yetu kubwa iwe ni kufanya kazi kwa kushirikiana, tupendane na kila mmoja akiwa na tatizo bila kujali nafasi yake aliyo nayo basi tushikamane katika kutatua tatizo. Nimefurahi sana kwa sababu pote nilipopita katika Idara na Vitengo nimejionea kile Katibu alichonieleza kuwa mnachapa kazi. Najua wengine mmekuja hapa Dodoma makazi yenu bado yako kwingineko lakini aliyepo jirani hapa ndio ndugu yako, aliyepo Ofisi nyingine pia ni ndugu yako mshikamane” alifafanua Jaji Mstaafu Mheshimiwa Kalombola.

“Mimi ninatoka hapa nikifahamu kuwa ninyi ni wachapa kazi na ninaomba na mimi mnipe ushirikiano, tuchape kazi pamoja na kama kuna changamoto tuendelee kuchapa kazi, wakati Viongozi na mimi mwenyewe tukizishughulikia. Tukichapa kazi ni vizuri maana hata kama tunaenda kuomba watu wengine watusaidie, watatusaidia kwa sababu tunaonekana tunafanya kazi na wanaona matokeo ya kazi zetu” alisema Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama alimhakikishia Mwenyekiti wa Tume kuwa yeye na Sekretarieti yake wataendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi na alimhakikishia ushirikiano.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nikuhakikishie kuwa tupo kwa ajili ya kuiwezesha Tume yako kufanya kazi zake vizuri. Wafanyakazi wa Tume wanafanya kazi zao vizuri, kielelezo kizuri kuona kiwango cha kazi zao ni kuangalia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa na kutolewa uamuzi na Tume. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Tume na pale mtakapoona pana upungufu mtaelekeza ili tuboreshe zaidi katika utendaji wa kazi zetu”

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages