Breaking

Wednesday 8 June 2022

WANAFUNZI WA VYUO WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA VITENDO VYA UKATILI



Na Ayoub Julius , Lango la habari 


Wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati Mkoani Mwanza wametakiwa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa au kuona Vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike katika mdahalo uliofanyika leo Jumatano Juni 08, 2022  katika chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino Jijini Mwanza ulioandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali Wadada Solutions  wenye lengo la kutoa elimu juu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.


Mdahalo huo umehusisha vyuo takribani vinne vilivyopo Jijini Mwanza ikiwemo chuo cha St. Augustine University of Tanzania, (SAUT), T.I.A,CBE na Chuo Cha Mipango huku ukiongozwa na kauli mbiu ulioongozwa na Mada "umuhimu wa afya ya uzazi na kupinga vitendo vya ukatili kwa ustawi wa vijana na maendeleo ya taifa"

RAS Samike amewataka wanafunzi hao kutoa taarifa za vitendo vya kikatili na unyayasaji wa kijinsia wanavyofanyiwa ama kuviona katika maeneo yao ili kuisaidia Serikali kupambana na matukio hayo.


Amesema kuwa wapo baadhi ya wanafunzi wanafanyiwa vitendo vya kikatili lakini hawatoi taarifa hali inayopeleka kupata athari za Kimwili, kiafya na kisaikolojia na kutokuwa na ufaulu mzuri darasani. 


"Unapofanyiwa kitendo cha ukatili usivumilie maana itakuathiri kisaikolojia huenda hata maksi utakazopata darasani si zako ungeweza kufanya vizuri darasani lakini kutokana na vitendo unavyofanyiwa na hutoi taarifa labda unatishiwa hii itakuathiri sana, jitahidi kutoa taarifa tafta njia ya kutoka" Amesema RAS Samike


Ameongeza kuwa uongozi wa Mkoa wa Mwanza utatoa muongozo kwa Vyuo ili kutoa elimu ya uzazi wa mpango ili kuwasaidia wanafunzi hasa wa mwaka wa kwanza ili kuepuka na vishawishi vitakavyopelekea ukatili wa kijinsia.


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa shirika la Wadada Solution, Lucy John amesema kuwa wanafunzi wanatakiwa kutambua uwepo wa madawati ya kijinsia katika taasisi zao na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa ili waweze kusaidiwa.


Naye Rais wa Serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino Festo Daffi amesema kuwa Serikali inatakiwa kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu juu ya vitendo hvyo ili jamii ziweze kutambua aina na namna unyanyasaji unavyofanyika hususani katika ngazi za elimu ya shule za msingi,sekondari na taasisi za elimu ya juu. 


Matukio ya ukatili na unyayasaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ulawiti na mauaji yamekuwa yakiongeza kasi katika Siku za hivi karibuni  Nchini Tanzania ambapo Serikali imeendelea kupambana navyo ikiwemo kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages