Dodoma
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya I. Samamba amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imetilia mkazo ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini (Local Content) na wajibu wa makampuni ya madini kutoa huduma kwenye jamii inayozunguka migodi (CSR).
Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Juni 02, 2022 katika Ofisi za Tume ya Madini Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu fursa zilizopo kwa Watanzania kwenye Sekta ya Madini.
Amesema kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazowekezwa katika Sekta ya Madini zinakwenda kwenye maeneo ya manunuzi na kutoa huduma kwenye masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini (Local Content) na kwenye miradi ya kijamii (CSR)
“Nachukua fursa hii kuwaambia Watanzania wenzangu hasa vijana kuhakikisha kwamba tunachangamkia fursa zilizopo katika utoaji wa huduma katika kampuni za madini (Local Content) kwa maana ya manunuzi, ajira, mafunzo na teknolojia inayopatikana kupitia uwekezaji kwenye Sekta ya Madini.
Ameeleza kuwa, Serikali iliyopo madarakani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia ilani yake ya mwaka 2025 iliahidi kutoa ajira kwa vijana na Watanzania kwa ujumla na kuwataka kuchangamkia fursa zilizopo nchini.
“Ajira hizo ni pamoja na kutoa huduma ya chakula, ulizi, huduma ya usafi kwenye migodi , huduma za baruti, na kuuza vipuli ambapo zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanatakiwa kuendesha mitambo ya kuchoronga, kupakia vifusi vya mchanga wenye madini na kupeleka kwenye maeneo ya uchenjuaji, amesema Mhandisi Samamba”
Ameeleza kuwa lengo la serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa vijana na wananchi wake na kuhimiza kuchangamkia fursa za kupata mikopo nafuu kwenye Taasisi za Fedha pamoja na kupata maelezo zaidi ya nafasi, ajira na fursa zilizopo kwenye migodi katika Ofisi 31 za Tume ya madini zilizopo nchini.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amesema kuwa kupitia filamu ya Royal Tour iliyotengenezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini na kujitangaza kimataifa, imeweka mazingira mazuri kwa Watanzania kwa ujumla kutumia fursa hiyo ya kuwakaribisha wawekezaji na kushirikiana nao kwa uaminifu ili kunufaika na Sekta ya
Aidha, Mhandisi Samamba amesema kuwa, Serikali inaelekeza jamii inayozunguka migodi kukaa pamoja na wawekezaji ili kuibua miradi ambayo inaigusa jamii moja kwa moja kama vile miradi ya maji , elimu na mingine inyozunguka migodi.
“Tuna mafanikio makubwa katika maeneo hayo ambapo tuna miradi mikubwa katika mkoa wa Geita kama vile barabara za lami, mashule, hospitali na mradi mwingine wa Bulyanhulu uliojenga zahanati nzuri za kisasa katika Wilaya ya Kahama na Halmshauri ya Msalala ambapo maeneo yote haya jamii imeweza kunufaika na (CSR), amesema Mhandisi Samamba”
Katibu Mtendaji amemalizia kwa kusema kuwa jamii inanufaika hata baada ya miradi ya uchimbaji wa madini kuisha kwa kuwa inakuwa imezikuza sekta nyingine kama vile biashara na kilimo.