Breaking

Monday 27 June 2022

TAMISEMI YATOA MAAGIZO KWA HALMASHAURI ZOTE NCHINI




Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) anayeshughulikia afya Dkt. Grace Magembe ameagiza Halmashauri zote nchini ambazo zinatekeleza ujenzi wa miundombinu ya afya kuongeza kasi, kuimarisha usimamizi na uwajibikaji wa pamoja katika kusimamia ujenzi wa miundombinu hiyo ili utekelezaji ukamilike kwa wakati.

Akizungumza tarehe 26 Juni 2022 baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya Halmashauri ya Biharamulo na Muleba Dkt. Magembe amesema kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi katika Halmashauri hizo hairidhishi, hivyo pamoja na kuongeza kasi amezitaka Halmashauri zote nchini kuimarisha usimamizi wa miradi.

Pia ameziagiza Halmashauri hizo kuandaa mpango kazi harakishi utakaoanisha kazi za utekelezaji zilizobaki ili kuweza kukamilisha ujenzi ndani ya muda uliopangwa.

“Ili miradi hii iweze kukamilika, Wakurugenzi andaeni mpango kazi wa utekelezaji harakishi utakaoainisha kazi iliyobaki, inafanyika lini, nani muhusika ili kufikia tarehe tuliyokubaliana miradi yote iwe imekamilika" Magembe

Vilevile amezitaka timu za usimamizi za Halmashauri zilizoundwa na Wakuu idara na vitengo kutoa taarifa ya utekelezaji kila siku ili kuimarisha usimamizi na ufatiliaji.

"Timu za usimamizi katika Halmashauri husika fungueni daftari la kupokea taarifa za utekelezaji hii itarahisisha ufatiliaji na usimamizi" Dkt. Magembe

Dkt. Magembe ameielekeza Halmashauri ya Biharamulo kuwa na ushirikiano katika utekelezaji wa miradi baada ya kuonekana kuna mapungufu katika uratibu, ufuatiliaji na usimamizi wa miradi na inayopelekea miradi kuwa nyuma sana ya muda wa utekelezaji.

Nao madiwani wa Kata za Buganguzi Bw. Renatus Rumota na Diwani wa Kata ya Nshamba Bw. Gosbert Masilingi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya Buganguzi na Nshamba, wameahidi kuendelea kuhamasisha Jamii kushiriki katika miradi ya maendeleo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wa kata zao.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages