Breaking

Tuesday 28 June 2022

WAZIRI MKUU MGENI RASMI TAMASHA LA UTAMADUNI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Tamasha la kwanza la kihistoria la Utamaduni  kitaifa  Julai 2, 2022  Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.


Tamasha hilo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwenye Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro la kutaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa tamasha kubwa la kitaifa la utamaduni litakaloshirikisha mikoa yote ya Tanzania ili kutangaza hazina ya utamaduni wa makabila ya Tanzania Duniani.


Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa,  amefafanua kuwa tamasha hilo litaambatana na matembezi maalum ya kitamaduni (Utamaduni Carnival) katika jiji la Dar es Salaam ambayo yameandaliwa njia  maalum za kupita ikiwemo daraja la juu la Mfugale, Kijazi, Tanzanite na daraja la mwalimu Nyerere.


Amesema,  tamasha hilo litatoa fursa kwa  makabila yote  nchini kuonesha  tamaduni zao kupitia  ngoma na vyakula vya asili  ili kukuza utalii wa kiutamaduni.


Aidha, amewataka watanzania  kujitokeza kushiriki kwenye  tamasha hilo la kwanza la kitaifa ambalo licha ya kutoa  burudani,  litaonesha  vitu  muhimu vya kiutamaduni na kutoa fursa kwa wageni kujifunza.


Ameongeza  kuwa,   tamasha hilo litakuwa  la siku tatu ambapo siku  inayofuata ya Julai 3, 2022  itakuwa  na tukio maalum la  mirindimo  ya taarabu ambapo limeainishwa kama usiku wa taarabu utakaofanyika eneo la  ufukwe wa Coco Beach  maarufu kwa wachoma mihogo kuanzia saa 8:00 hadi saa 6:00 usiku.


Amesema shamrashamra hizo zitashamirishwa na vikundi mbalimbali vya wasanii kutoka ndani na nje ya Tanzania kama Comoro, Burundi na Kenya,  pia wasanii  wa taarabu nchini akiwemo  Mzee Yusufu, Hadija Kopa, Patricia Hillay, Abuduli Misambano na Aisha Mashauzi watakuwepo kutumbuiza usiku huo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages