Breaking

Friday 24 June 2022

ZANA ZA UVUVI HARAMU ZENYE THAMANI YA BILIONI 1.25 ZATEKETEZWA KWA MOTO KAGERA


Na Lydia Lugakila, Lango La Habari

Zana haramu za uvuvi zenye thamani ya Tsh. bilioni 1.25 zimeteketezwa kwa moto huku watuhumiwa 34 wakikamatwa katika Wilaya ya Muleba Mkoani Geita.


Zana hizo ni pamoja na kokoro 44, nyavu 11 zilizo chini ya inchi 6, timba 356 katuli 2 na Kamba za  kuvuta kokoro zenye urefu wa mita 810 ikiwa watuhumiwa waliokamatwa ni wavuvi 34.


Akizungumza katika uteketezaji wa zana hizo uliofanyika Alhamisi Juni 23, 2022 katika kijiji Katunguru, kata ya Gwanseli, Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ameendelea kuwasisitiza viongozi na wananchi kuwa mstari wa mbele kupambana kutokomeza uvuvi haramu ili kuwa na uvuvi endelevu wenye manufaa.


"Msikubali kamwe wavuvi haramu wakaendelea kuvua na timba na makokoro zana ambazo zinavua mpaka samaki wachanga tusipopambana na kuhakikisha tunawabaini wavuvi haramu na kuwachukulia hatua tutabaki na maji matupu bila samaki" amesema Mhe. Nguvila.


Dc Nguvila amesema kuwa uvuvi haramu ukitokomezwa wananchi wataweza kukuza uchumi  wao na biashara ya samaki itakua zaidi.


"Mfanyabiashara yeyote anayewaletea nyavu haramu huyo ni muuaji mkimuona mfanyabiashara anayewaletea nyavu haramu mtoe taarifa haraka ili achukuliwe hatua za kisheria" ameendelea kueleza Mhe. Nguvila.


Aidha, amewaasa wananchi kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na kuwaeleza kuwa Serikali tayari imetoa kipaumbele kwenye bajeti Kuu ya Serikali 2022/23 kuanzisha ufugaji wa samaki kwa vizimba hivyo kuwafanya wavuvi kufuga samaki na kuendela kunufaika na uvuvi halali.


Akisoma taarifa fupi kabla ya uteketezaji wa zana hizo, Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Wirfred Tibendelana amesema zoezi hilo ni mwendelezo wa kutokomeza uvuvi haramu kwa kuzingatia Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2020 ambazo zinamtaka mvuvi kutotumia zana haramu ikiwemo nyavu za chini ya inchi 6.


Naye Agripina Joas Matungwa, mkazi wa Katunguru ameonyesha kuchukizwa na uvuvi haramu na kueleza kuwa kutokana na uvuvi haramu samaki hawapatikani kama zamani hivyo ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa na kuhakikisha uvuvi haramu unatokomezwa katika Wilaya ya Muleba.

Mwisho

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages