Breaking

Monday 25 July 2022

MUME AMUUA MKEWE KWA KIPIGO WAKIWA FUNGATE



Mwanaume mmoja wa Nchini Marekani anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe walipokuwa kwenye fungate, ABC News imebaini.

Bradley Robert Dawson anatuhumiwa kumuua mkewe walipokuwa kwenye honeymoon (fungate) kwenye hoteli ya kifahari huko katika Visiwa vya Yasawa huko Fiji, Kusini mwa Bahari ya Pasifiki.

Jeshi la Polisi katika eneo hilo limethibitisha kuwa alasiri ya Julai 9, mwanamke aliyetambuliwa kuwa ni raia wa Marekani, Christe Chen mwenye umri wa miaka 36 alipatikana akiwa amefariki dunia kwenye sakafu ya chumba cha walichokodisha kwa ajili ya mapumziko baada ya kufunga ndoa.

Wafanyakazi wa hoteli hiyo waliwaambia Polisi kwamba Chen alifariki dunia baada ya kupigwa na mume wake wakiwa fungate.



Mume wa Chen aliyetambuliwa kama raia wa Marekani Bradley Robert Dawson mwenye umri wa miaka 38, alipatikana na kukamatwa siku mbili baadaye huko Nadi Pwani ya Magharibi ya Kisiwa Kikuu cha Fiji cha Viti Levu.

Dawson alifikishwa katika Mahakama ya Lautoka mnamo Julai 13 na kushtakiwa kwa kosa moja la mauaji.

Kutokana na uzito wa tukio hilo, kesi ya Dawson ilifikishwa Mahakama Kuu ya Lautoka, ambako imepangwa kutajwa Julai 27, 2022 ambapo anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha Huduma ya Marekebisho ya Fiji kilichopo Lautoka, jiji la pili kwa ukubwa nchini Fiji, takriban maili 16. kaskazini mwa Nadi.

Wakili wa Dawson, Iqbal Khan, aliiambia ABC News kuwa anakusudia kuwasilisha ombi la dhamana kwa niaba ya mteja wake Julai 25 lakini anaamini itakuwa vigumu kupata dhamana, kwa sababu Dawson ni mgeni na hana familia ya ndani au uhusiano ambao unaweza kutoa ushahidi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages